Rais Uhuru ampongeza rais wa Ufaransa Macron kwa kuchaguliwa tena

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta amempongeza mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kufuatia kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili afisini
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron kufuatia kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili afisini.

Rais Macron, 44, alipata zaidi ya asilimia 58 ya kura za wananchi akimshinda mpinzani wake Marie Le Pen katika marudio ya uchaguzi wa Jumapili.

Katikaujumbe wake wa pongezi, Uhuru alitaja ushindi huo mzuri wa Macron kama uthibitisho wa imani ya watu wa Ufaransa katika usimamizi wake wa nchi hiyo ya Ulaya.

"Pongezi za dhati kwako Mheshimiwa na kaka yangu mpendwa kwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili. Ushindi wako ni uthibitisho wa imani kubwa waliyo nayo wanaume na wanawake wenzako katika uongozi wako," Uhuru alisema.

Alimhakikishia Rais Macron kuhusu kujitolea kwa Kenya kuendelea kufanya kazi na Ufaransa kwa manufaa ya wote na ustawi wa Jamhuri hizo mbili.

“Unapotulia katika muhula wako wa pili afisini, ninakutakia afya njema na mafanikio unapoiongoza nchi yako pendwa kwenye kilele kipya cha ustawi,” Rais Uhuru aliongeza.