Wafuasi wa mbunge Tiren waandamana mjini Eldoret baada ya IEBC kutangaza anawania uwakilishi wadi

Muhtasari
  • Wafuasi wa mbunge Tiren waandamana mjini Eldoret baada ya IEBC kutangaza anawania uwakilishi wadi

Wafuasi wa mbunge wa Moiben Sila Tiren walifanya maandamano mjini Eldoret baada ya IEBC kutangaza jina lake kama mgombea wa kiti cha uwakilishi wadi badala ya ubunge.

Tiren anatetea kiti chake ambacho kiko Uasin Gishu kama mgombeaji huru lakini IEBC ilimtaja kama mgombeaji kiti cha wadi ya Moiben.

Mbunge huyo alipiga kambi katika IEBC ili suala hilo lirekebishwe hata wafuasi wake walipoandamana mjini Eldoret.

Wafuasi hao wakiongozwa na Julius Korir walitishia kuvamia afisi za IEBC mjini Eldoret ili kosa hilo lirekebishwe.

“Tunaomba IEBC ihakikishe kuwa mbunge wetu anamiliki mali iliyotangazwa kwenye gazeti la serikali kama mwaniaji ubunge na wala si mwakilishi wadi.

Korir alisema Tiren alikuwa mbunge mara ya pili na kudai kuwa kosa hilo litawachanganya baadhi ya wafuasi wake.

Tiren anachuana dhidi ya mteuliwa wa UDA wa eneo hilo Profesa Phyllis Bartoo na mbunge wa zamani Joseph Lagat ambaye pia anawania kama mwaniaji huru.

Wafuasi wa Tiren walibeba mabango wakitaka IEBC ichukuliwe hatua za haraka.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu kilimo alithibitisha kuwa alikuwa katika IEBC akitaka tatizo hilo kurekebishwa.

"Ninatumai kuwa mamakosa hayo yatarekebishwa haraka kabla ya muda kuisha," Tiren alisema.

Wafuasi wake walitishia kwenda mahakamani kusitisha uchaguzi wa Moiben iwapo kosa hilo halitarekebishwa na IEBC.