IPOA kuchunguza vifo vya waandamanaji wanne wanaodaiwa kuuawa na polisi Kajiado

Muhtasari

•IPOA imesema uchunguzi ulianzishwa Ijumaa asubuhi ili kubaini matukio yanayozingira tukio hilo la kutisha.

•Sheria zinazoongoza polisi zinasema kuwa maafisa wanapaswa kutumia njia zisizo za hatia dhidi ya waandamanaji.

Waandamanaji eneo la Masimba kando ya barabara kuu ya Nairobi-Mombasa kabla ya maafisa wa GSU kufika na wanadaiwa kuwafyatulia risasi na kuwaua wanne na kujeruhi saba.
Waandamanaji eneo la Masimba kando ya barabara kuu ya Nairobi-Mombasa kabla ya maafisa wa GSU kufika na wanadaiwa kuwafyatulia risasi na kuwaua wanne na kujeruhi saba.
Image: KURGAT MARINDANY

Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA)  imeahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kisa ambapo polisi wanadaiwa kupiga risasi na kuua watu wanne miongoni mwa kundi lililokuwa linaandamana Alhamisi katika eneo la Kajiado. 

Jumla ya watu wanne wanaripotiwa kupoteza uhai huku wengine saba wakijeruhiwa baada ya wanawake waliokuwa wakiandamana kulalamika dhidi ya wanyamapori kufunga barabara katika juhudi za kusitisha uvamizi wa wanyamapori.

IPOA imesema uchunguzi ulianzishwa Ijumaa asubuhi ili kubaini matukio yanayozingira tukio hilo la kutisha.

"Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, ambapo kosa limepatikana, mamlaka itatoa mapendekezo, ikiwa ni pamoja na kushtakiwa," Taarifa iliyotilewa na mamlaka hiyo ilisoma.

Alhamisi kundi la wanawake liliandamana likitoa wito wa kuchukuliwa hatua dhidi ya migogoro  kati ya binadamu na wanyamapori wakati maafisa wa GSU walipofyatua risasi na kuwaua wanne papo hapo.Wengine saba walijeruhiwa.

Kundi hilo la wanawake lilikuwa limeandaa maandamano kuonyesha hasira zao kufuatia kifo cha mwalimu aliyeripotiwa kuuawa na tembo.

Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku alikashifu utumizi wa risasi na maafisa wa usalama kutawanya maandamano hayo.

Huku akiwafariji wanafamilia wa watu wanne waliouawa, Lenku alilaani kitendo cha polisi na kuongeza kuwa hawakupaswa kutumia risasi dhidi ya waandamanaji hao wasio na hatia.

"Ninatuma rambirambi zangu kwa familia za watu wanne ambao wameuawa kwa kupigwa risasi Masimba, kando ya barabara kuu ya Nairobi-Mombasa, wakati wa ugomvi kuhusu kuongezeka kwa mauaji ya watu na wanyamapori huko Kajiado Mashariki," Gavana Lenku alisema.

Sheria zinazoongoza polisi zinasema kuwa maafisa wanapaswa kutumia njia zisizo za hatia dhidi ya waandamanaji.

Polisi anayetumia nguvu zaidi anapaswa kuripoti kwa wakubwa wake na hatua kali inafaa kuchukuliwa iwapo atakosa kufanya vile.