Hutaepuka haya,tunajua kinachoendelea-Wanjigi amwambia Chebukati

Muhtasari
  • Chebukati alizima kipasa sauti Wanjigi alipozidisha maandamano yake kufuatia uamuzi wa kumnyima kibali
(Kushoto)Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati,(Kulia)Mwaniaji urais Jimi Wanjigi wakiwa Bomas of Kenya 06/006/2022
Image: WILFRED NYANGARESI

Mgombea urais wa Safina Jimi Wanjigi amesema atatumia njia zote za kisheria na kuhakikisha atashiriki kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Akizungumza Jumatatu baada ya kunyimwa kibali na IEBC katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Wanjigi alimlaumu mwenyekiti Wafula Chebukati kwa kutumia viwango viwili katika kuwaidhinisha wagombeaji.

"Tunajua kinachoendelea, na kwa bahati mbaya wakati huu hutaepuka," Wanjigi alisema.

"Inaonekana kuna uamuzi wazi kwamba kuna watu ambao hawafai kuwa kwenye kura, na mimi ni mmoja wao," aliongeza.

Chebukati alizima kipasa sauti Wanjigi alipozidisha maandamano yake kufuatia uamuzi wa kumnyima kibali.

"Tafadhali hutubia wafuasi wako kutoka nje," Chebukati alisema kwa uthabiti.

Bosi huyo wa baraza la uchaguzi alimwambia Wanjigi kuwa aliwasilisha saini za kutosha za watu wanaomuunga mkono, pungufu ya kaunti moja.

Pia alishindwa kuwasilisha nakala halisi ya shahada yake ya chuo kikuu.

Wagombea urais walitakiwa kuwasilisha sahihi za wafuasi ambao wameidhinisha azma yao ya urais kutoka kaunti 24 nyingi.