"Hakuna likizo kwa maafisa wa polisi!" - Hillary Mutyambai

Barua iliyotumwa kwa makamanda wa mikoa na naibu inspekta jenerali iliwataka maafisa wote walioko likizoni kurejea kazini.

Muhtasari

• "Maafisa wote waliokuwa likizoni wataitwa na kuwa kazini ifikapo tarehe 4 Julai 2022,” - IG

Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai
Image: George Owiti

Inspekta jenerali wa polisi Hillary Mutyambai amesitisha mipango yote ya kuwapa maafisa wa polisi likizo hadi baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kulingana na taarifa iliyopakiwa kwenye ukurasa wa Facebook wa tume ya huduma kwa polisi NPS kutoka kwa gazeti moja la humu nchini, inaarifiwa kwamba naibu inspekta jenerali wa polisi, Edward Mbugua alituma kumbukumbu kwa makamanda wa mikoa na kuwataka waarifu maafisa wote wa polisi walioko kwenye likizo kurejea kazini mara moja.

Kumbukumbu hiyo iliwapa maafisa walioko kwenye likizo hadi Julai 4 wawe wamerejelea majukumu yao kama kawaida.

“Kutokana na uchaguzi mkuu ujao, hakuna afisa anayepaswa kupewa likizo kuanzia Julai 1, 2022, isipokuwa kwa misingi ya matibabu na mapendekezo ya madaktari. Maafisa wote waliokuwa likizoni wataitwa na kuwa kazini ifikapo tarehe 4 Julai 2022,” gazeti hilo lilinukuu kumbukumbu hiyo.

Maafisa wa polisi wamekuwa wakipewa mafunzo jinsi ya kusaidia tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kuendesha uchaguzi kwa amani bila vurugu zozote.

Juzi Waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’I aliwataka walimu na polisi kujiepusha na siasa za marengo taifa linapojiandaa kuelekeqa uchaguzi mkuu wa Agosti 9 na kuwataka kukoma kushiriki katika vitendo vya kisiasa kwa sababu wao vi watoa huduma kwa umma na hivyo hawafai kuonesha wazi marengo wanayoipendelea.