Wanandoa wakamatwa kwa kuishi na maiti wakitarajia itafufuka tena Kirinyaga

Wanakijiji hao walioshtuka walisema walitatanishwa na jinsi familia hiyo ilivyofanikiwa kuishi na maiti hiyo licha ya kuwa na harufu mbaya nyumbani kwao.

Muhtasari
  • Wanandoa wakamatwa kwa kuishi na maiti wakitarajia itafufuka tena Kirinyaga
Pingu
Image: Radio Jambo

James Muchira, 45 na mkewe wamekamatwa kwa kuishi na maiti ya mamake. Wanandoa hao wa Kirinyaga walifikiri kumuombea mwanamke aliyekufa kungemfufua, kwa hivyo akaweka mwili wake nyumbani.

James Muchira na mkewe walinaswa katika kijiji cha Mutithi Jumatatu usiku baada ya jamaa zake, wakiongozwa na kakake Evans Mwaniki, kumtaka chifu msaidizi wa eneo hilo kujihusisha, kulingana na kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Mwea-Magharibi Wilson Koskei.

Kulingana na ripoti, mshukiwa alikataa kuruhusu mtu yeyote ndani ya nyumba yake, ambayo pia hutumika kama kanisa linalojulikana kama "mlima wa Mungu wa waumini."

"Maafisa wangu walishtuka kugundua mwili uliooza," Koskei aliambia Citizen Digital

Mshukiwa huyo anadaiwa kumchukua mamake kutoka hospitali alikokuwa akipokea huduma ili aweze kumuombea katika kanisa lake la nyumbani.

Wanakijiji hao walioshtuka walisema walitatanishwa na jinsi familia hiyo ilivyofanikiwa kuishi na maiti hiyo licha ya kuwa na harufu mbaya nyumbani kwao.

"Hili si kanisa bali ni dhehebu," Lucy Njeri, jirani alisema.

Ili kuwalinda dhidi ya watu waliokuwa wamekasirika waliotaka kuwaua, Muchira, mkewe na mwanamke mwingine walipelekwa haraka katika kituo cha polisi cha Kiamaciri.

Mwili wa Tabitha Wakathare ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kerugoya ukisubiri uchunguzi wa maiti.