Si Haki kumlaumu Uhuru kwa gharama ya juu ya maisha-Oguna

Msemaji huyo aliongeza kwa taarifa yake kuwa hali ya sasa haina tofauti katika nchi jirani.

Muhtasari
  • “Kuna nchi jirani ambapo rais aliwaambia wananchi watarajie gharama ya juu ya maisha na wakaelewa, lakini hapa tunamlaumu Uhuru,” Oguna aliongeza.
Msemaji wa Serikali Cyrus Oguna

Msemaji wa serikali Cyrus Oguna amesema Kenya inafaa kukoma kumlaumu rais kwa gharama ya juu ya maisha.

Katika mahojiano na Radio Citizen siku ya Jumatano Oguna alisema gharama ya juu ya maisha inatokana na mzozo wa Ukraine - Urusi.

"Si haki kulaumu hali nzima kwa mtu binafsi, kwa sababu si rahisi kila mahali," alisema.

Oguna alisema rais hana udhibiti wa hali iliyopo.

Oguna alitaja mambo mengine mbalimbali yanayochangia kuongezeka kwa gharama ya maisha kama vile janga la Covid-19, ukame wa muda mrefu, mzozo wa Ukraine na Urusi na kuendelea kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Marekani.

Msemaji huyo aliongeza kwa taarifa yake kuwa hali ya sasa haina tofauti katika nchi jirani.

“Kuna nchi jirani ambapo rais aliwaambia wananchi watarajie gharama ya juu ya maisha na wakaelewa, lakini hapa tunamlaumu Uhuru,” Oguna aliongeza.

“Kwa kweli nimezungumza na Rais kuhusu masuala haya. Najua anakabiliwa na changamoto nyingi, sasa serikali inavutwa pande mbili tofauti; kuna kundi la serikali ambalo linapinga ajenda ya serikali," alisema.

Alisema serikali inapaswa kupewa muda kwa ajili ya mipango inayoendelea kuanza kutoa matokeo yanayoonekana.