Mwanamume apatikana amekufa katika makazi yake Machakos

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Athi River waliuondoa mwili huo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Machakos Level 5.

Muhtasari
  • Mwanamume apatikana amekufa katika makazi yake Machakos
  • Maafisa wa DCI kutoka kituo hicho wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo
Image: GEORGE OWITI

Mwanamume mmoja amepatikana akiwa amefariki katika nyumba iliyotelekezwa inayoshukiwa kuwa makazi yake huko Athi River, Kaunti ya Machakos.

Chifu msaidizi wa Athi River Martin Ngomo alisema mwili huo uligunduliwa katika nyumba hiyo iliyotelekezwa na wapita njia mwendo wa saa 11.00 asubuhi Alhamisi.

Nyumba ambayo mwili huo ulipatikana ukiwa katika shamba la Embakasi haina paa wala milango.

"Tulipokea simu mwendo wa saa 10.00 asubuhi kwamba kulikuwa na kijana aliyeungua. Aliteketea kiasi cha kutotambulika katika eneo la mji wa Athi River ndani ya kaunti ndogo ya Athi River," Ngomo aliambia Radiojambo katika eneo la tukio Alhamisi.

Msimamizi huyo alisema marehemu alikuwa mwendawazimu kabla ya kuchomwa moto.

Ngomo alisema mtu huyo anafahamika sana na wakazi kwa jina la utani, profesa.

Aliwaambia wakazi kuwa waangalifu hasa wanapotumia moto.

Inashukiwa kuwa godoro alilokuwa amelalia iliwaka  moto na kusababisha kifo chake.

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Athi River waliuondoa mwili huo hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Machakos Level 5.

Sababu ya moto haikujulikana mara moja.

Maafisa wa DCI kutoka kituo hicho wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.