Rais Kenyatta atuzwa na Burundi kwa kukuza amani, usalama na utulivu

Tuzo hiyo ya heshima alikabidhiwa Rais Kenyatta na Rais Evariste Ndayishimiye wakati wa sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Burundi zilizofanyika Julai 1 mjini Bujumbura

Muhtasari
  • Rais Uhuru Kenyatta ametuzwa kwa jukumu lake bora katika kukuza amani, usalama na utulivu nchini Burundi na eneo la Maziwa Makuu kwa jumla
Rais Kenyatta atuzwa na Burundi kwa kukuza amani, usalama na utulivu
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametuzwa kwa jukumu lake bora katika kukuza amani, usalama na utulivu nchini Burundi na eneo la Maziwa Makuu kwa jumla.

Rais Kenyatta amepokea Tuzo ya Kitaifa ya Jamhuri ya Burundi, tuzo ya juu zaidi ya heshima katika taifa hilo la Afrika Mashariki, leo katika Ikulu ya Nairobi.

Tuzo hiyo ya heshima alikabidhiwa Rais Kenyatta na Rais Evariste Ndayishimiye wakati wa sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Burundi zilizofanyika Julai 1 mjini Bujumbura ambapo Balozi wa Kenya nchini Burundi Daniel Waisiko Wambura aliipokea kwa niaba ya Mkuu wa Nchi ya Kenya na kuikabidhi kwake leo.

Dondoo hilo lilisema kuwa Rais Kenyatta alitunukiwa kwa jukumu lake kubwa la kukuza amani, usalama na utulivu nchini Burundi wakati wa mzozo wa kisiasa mwaka wa 2015.

"Jukumu muhimu la Serikali ya Kenya katika kufanya kampeni kwa mafanikio ya kuondolewa kwa Burundi katika orodha ya waangalizi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," ilisema sehemu ya nukuu hiyo.

Tuzo hilo pia lilitambua uungwaji mkono wa kibinafsi, ushirikiano na mshikamano wa Rais Kenyatta katika kufanikisha kampeni ya kutaka vikwazo vilivyowekewa Burundi na Umoja wa Ulaya na washirika wengine wa maendeleo kuondolewa.