Bunduki ya polisi iliyoibwa wakati wa wizi wa benki Matuu yapatikana Kiambu

Mmiliki wa shamba hilo aliwaambia polisi kuwa alikuwa akifyeka kichaka alipojikwaa na silaha hiyo.

Muhtasari
  • Bunduki ya AK47 ilipatikana kwenye kichaka katika shamba la kibinafsi mnamo Julai 7, 2022, karibu mwaka mmoja baada ya kuibiwa
  • Risasi tisa zilikosekana kutoka kwa 30 zilizokuwemo wakati ilipoibiwa
Bunduki ya polisi iliyoibwa wakati wa wizi wa benki Matuu yapatikana Kiambu
Image: DCI/TWITTER

Bunduki iliyoibwa kutoka kwa maafisa wawili wa polisi wakati wa kisa cha wizi katika tawi la Matuu Equity, Machakos, imepatikana katika kichaka cha Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Bunduki ya AK47 ilipatikana kwenye kichaka katika shamba la kibinafsi mnamo Julai 7, 2022, karibu mwaka mmoja baada ya kuibiwa.

Mmiliki wa shamba hilo aliwaambia polisi kuwa alikuwa akifyeka kichaka alipojikwaa na silaha hiyo.

Silaha hiyo nambari KE KP 55266385 ilipatikana ikiwa na risasi 21 kwenye kichaka na ilikuwa katika hali inayoweza kutumika wakati huo, polisi walisema.

Risasi tisa zilikosekana kutoka kwa 30 zilizokuwemo wakati ilipoibiwa.

Hakuna aliyekamatwa na haijafahamika ni muda gani imekaa eneo la tukio.

Ilinyakuliwa kutoka kwa konstebo Patrick Omusebe mnamo Julai 27, 2021, wakati wa kisa cha wizi mkali katika benki na watu watano wanaoshukiwa kuwa majambazi.

Silaha hiyo ilipelekwa kwa Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ili kubaini iwapo imetumika katika mashambulizi yoyote.

Katika kisa hicho, walioshuhudia na polisi walisema genge la watu watatu liliwavamia kwanza maafisa wawili wa polisi waliokuwa zamu katika kituo hicho na kunyakua bunduki zao kabla ya kuvamia benki.

Wakaamuru baadhi ya wafanyakazi na wateja waliokuwepo kulala chini.

Ukaguzi wa picha za CCTV ulionyesha mmoja wa maafisa waliokuwa wakisimamia benki hiyo, Konstebo Dorothy Opili, akitoka kwenye  kiti chake nje ya majengo muda mfupi kabla ya wizi huo.

Alipoondoka, aliacha bunduki aina ya AK-47, nambari 5527115 na kubeba risasi 30 pamoja na mwenzake, Omusebe.

Afisa huyo wa kiume alikuwa na AK47 yake, nambari 5526385, ambayo pia ilikuwa na risasi 30. Muda mfupi, aliweka bunduki zote mbili sakafuni na kuketi.

Picha zilionyesha genge hilo lliliwasili saa tatu kamili asubuhi wakati benki ilikuwa imefunguliwa.