VC wa chuo cha KU ajiuzulu siku chache baada ya rais Kenyatta kufoka

Rais Kenyatta alisema katika wiki 3 alizo nazo ofisini atahakikisha ameenda na baadhi ya wakosoaji wake nyumbani.

Muhtasari

• Inasemekana VC huyo aliwaambia wanafunzi kwanza amepumuzishwa majukumu yake kama VC wa chuo hicho.

VC wa chuo kikuu cha Kenyatta, profesa Paul Wainaina
VC wa chuo kikuu cha Kenyatta, profesa Paul Wainaina
Image: Enos Teche (The Star)

Mkuu wa chuo cha Kenyatta, profesa Paul Wainaina amejiuzulu wadhifa wake kama VC wa chuo hicho, wiki moja tu baada ya kuvurugana na rais Uhuru Kenyatta kutokana na mzozo wa shamba la chuo hicho ambacho maabara ya WHO yalikuwa yanajengwa.

Usimamizi wa chuo hicho kilichoko barabara kuu ya Thika ulikuwa umelalama kwamba maabara hiyo ya WHO ilikuwa imejengwa pasi na usimamizi kushirikishwa ambapo walisema eneo hilo lilikuwa limetengwa kwa maendele mengine ya chuo.

Wikendi iliyopita wakati rais Kenyatta aliwasuta vikali wasimamizi hao huku akisema shamba hilo ambako mradi huo ulikuwa unajengwa ni miliki ya wananchi, na kusema kwamba bado ana wiki kama tatu ofisini kama rais ambazo atatumia kuhakikisha wale wote wanaopinga miradi kama hiyo wataenda naye nyumbani.

“Shamba liwe ni lile la ikulu ambapo mimi ninakaa kwa wiki chache zijazo, ama ni chuo ama hospitali, mashamba haya yote ni miliki za wananchi ambayo yamewekwa mikononi mwa serikali. Ndio maana tunajaribu kuchukua mwelekeo wa kiserikali zaidi katika kuyatumia,” alisema rais Kenyatta kwa ghadhabu kubwa.

Siku chache baadae, ni kama wameanza hata kumtangulia kuenda nyumbani, ambapo taarifa zinaripoti kwamba VC wa chuo hicho ambaye alikuwa mstari wa mbele kupinga kujengwa kwa maabara hiyo ashajiuzulu.

Kulingana na taarifa zilizosambazwa kutoka chuoni humo, profesa Wainaiana aliwataarifu wanafunzi kwamba amepumzishwa kutoka kwa majukumu yake na baada ya usimamizi wa chuo kukataa kuachia shamba kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa shirika la afya duniani, WHO