Kakuma kupewa hadhi ya manispaa kuvutia wawekezaji

Mji wa Kakuma ni wa pili kwa ukubwa kwenye kaunti ya Turkana baada ya Lodwar

Muhtasari

• Mji wa Kakuma ulijulikana haswa kutokana na wakimbizi wengi kutoka Sudan Kusini kuufanya kuwa makaazi yao baada ya kutoroka Sudan.

Mji wa kakuma kwenye kaunti ya Turkana
Mji wa kakuma kwenye kaunti ya Turkana
Image: YouTube (screenshot)

Ni taarifa njema kwa wakaazi wa kaunti ya Turkana haswa wakaazi wa eneo la Kakuma ambapo sasa eneo hilo linatarajiwa kupandishwa hadhi hadi kiwango cha manispaa ili kuwavutia wawekezaji.

Taarifa zinasema kwamba serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na shirika la umoja wa mataifa linalosimamia mazingira, UN-Habitat wameafikiana kuboresha zaidi miundo msingi na miundo mbinu kwenye eneo hilo ili kuupandisha mji wa Kakuma mpaka hadhi ya manispaa.

Eneo la Kakuma lilianza kukua kutokana na wakimbizi wengi wao wakiwa wale waliokuwa wakikimbia ghasia za vita vya wenyewe kwa wenyewe kutoka nchi Jirani ya Sudan Kusini.

Kulingana na taarifa kutoka kwa afisa mwandaizi wa program za UN-Habitat Ivan Unluova, kama ilivyonukuliwa katika chapisho moja la humu nchini, maafikiano hayo yanalenga kuvutia wawekezaji zaidi katika kaunti hiyo ya jangwani na Kakuma sasa utakuwa mji wa pili wenye hadhi ya kimanispaa baada ya Lodwar.

Kitengo kinachosimamia wahamiaji na wakimbizi UNHCR kimeanzisha mpango wa kubadilisha hadhi ya miji na maeneo ambayo yamewaweka wakimbizi kuwa miji ya manispaa ili kuboresha maisha ya wakimbizi hao ambao wengi wanaishi maisha mabaya sana, haswa katika hema za wakimbizi zenye hadhi ya kimaskini mno.

Kakuma ambayo wengi walipata kuisikia kwa mara ya kwanza wakati wa wakimbizi kutoka Sudan Kusini kwa sasa imeimarika pakubwa huku maendeo kadhaa yakionekana katika eneo hilo linalokadiliwa kuwa na zaidi ya wakaazi takribani laki mbili, na wengi wanasema ukuaji huu ni kutokana na ujio wa ujenzi wa barabara kuu inayounganisha Kenya na Sudan Kusini kupitia sehemu za Lodwar, Kakuma, Lokichoggio kuelekea Sudan ya Kusini.