Paul Muite akanusha vikali taarifa kwamba anaugua saratani

Watu walizua gumzo mitandaoni kwamba anaugua saratani kutokana na picha iliyomuonesha kapungua uzito wa mwili.

Muhtasari

• Muite alisema aliamua tu kupunguza uzito wa mwili ili kujiweka sawa kiafya kutokaan na umri wake ulivyosonga.

• Alisema wakati watu wanasema anaugua saratani yeye alikuwa katika msitu wa Ngong kufanya mazoezi ya kukimbia.

Mshauri mkuu wa masuala ya kisheria Paul Muite.
Mshauri mkuu wa masuala ya kisheria Paul Muite.
Image: Facebook

Mshauri mkuu wa masuala ya kisheria na ambaye aliwahi gombea nyadhifa ya urais nchini Kenya, Paul Muite amejitokeza kimasomaso na kupuuzilia mbali madai ambayo yamesambazwa mitandaoni Ijumaa kwamab anaugua ugonjwa wa saratani kutokana na picha yake aliyoonekana kudhoofika na baadhi ya nywele kupotea kichwani.

Muite ni kinara na mwanzilishi wa chama cha SAFINA ambacho mkwasi Jimmy Wanjigi alilenga kukitumia kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kabla ya tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC kumzuai kwa kukosa vyeti maalum na vigezo vingine vilivyohitajika na tume hiyo ili mtu kuruhusiwa kuwania kama rais.

Ijumaa adhuhuri baadhi ya makundi ya mitandaoni na wanablogu baada ya kuona picha hiyo yake walizua madai kwamba anaugua kansa na mpaka kuanza kumtakia nafuu ya haraka huku wakikemea saratani bila aibu wala soni.

Muite alicharuka kwenye ukurasa wake wa Twitter ambapo alipuuzilia madai hayo na kusema yeye yupo salama tena katika hali shwari ya kiafya na kusema kwamba nywele hupotea tu kutokana na umri wake kusonga sana.

Muite pia aliwasuta wanaosema anaugua kansa kutokana na kupungua kwa uzito wa mwili wake na kusema kwamba kutokana na umri wake mkubwa alilazimika kufanya mazoezi ya kupunguza uzito ili kujilinda kutokana na magonjwa kama kisukari na mengine yanayohusiana na afya.

“Taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ninaumwa na saratani SI ZA UKWELI. Kwa kuzingatia umri wangu, imenilazimu kupunguza uzito makusudi ili kuweka viwango vya sukari mahali panapopaswa kuwa. Vinginevyo sijawahi kujisikia vizuri; nilifurahia kukimbia kwa saa 1 na nusu katika msitu wa Ngong leo asubuhi,” Muiti aliandika na kumalizia kwa emoji ya kicheko.