Rais Kenyatta amuomboleza dadake hayati Mwai Kibaki

Bi Waitherero alifariki akiwa na umri wa miaka 115.

Muhtasari

•Bi Esther Waitherero aliaga dunia Alhamisi asubuhi nyumbani kwake katika kijiji cha Gatuyaini, eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri.

•Rais Kenyatta alimsifu marehemu kama nguzo imara katika maisha ya aliyekuwa rais wa tatu, hayati Kibaki na nanga ya familia yote ya Kibaki.

akiwa ameshikilia picha yenye picha ya rais wa tatu wa Kenya marehemu Mwai Kibak
Dadake marehemu Mwai Kibaki Esther Waitherero akiwa ameshikilia picha yenye picha ya rais wa tatu wa Kenya marehemu Mwai Kibak
Image: HISANI

Rais Uhuru Kenyatta ameifariji familia ya aliyekuwa rais wa tatu Mwai Kibaki kufuatia kifo cha dadake mkubwa Esther Waitherero.

Bi Waitherero, ambaye alikuwa ndugu pekee wa Kibaki aliyesalia aliaga dunia Alhamisi asubuhi nyumbani kwake katika kijiji cha Gatuyaini, eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri.

Huku akimuomboleza, Rais Kenyatta alimtaja marehemu Waitherero kuwa mwanamke shupavu, kielelezo cha jamii na shujaa wa kupigania uhuru wa Kenya.

"Inasikitisha kwamba tumepoteza mmoja wa watetezi wa mstari wa mbele wa uhuru wa nchi yetu alikuwa amesalia. Mama Waitherero alilipa gharama kubwa kwa uhuru wa Kenya wakati alipompoteza mumewe katika ghasia za Mau Mau dhidi ya utawala wa kikoloni," Rais Kenyatta alisema.

Aliongeza "Kama taifa la Kenya lenye shukrani, tuna deni la shukrani kwa Mama Waitherero na kizazi chake cha wanawake wenye nguvu ambao walipigana pamoja na wenzao wa kiume katika mapambano ya ukombozi wa nchi yetu."

Uhuru alisema Bi Waitherero atakumbukwa daima katika historia ya taifa kama shujaa, kwa jukumu la kipekee katika kuunda taifa la Kenya.

Rais pia alimtaja marehemu kama shujaa aliyewafungulia njia wanawake wengine wakubwa wa Kenya.

Rais alimsifu marehemu kama nguzo imara katika maisha ya marehemu rais mstaafu hayati Mwai Kibaki, na nanga ya familia ya Kibaki.

"Katika maisha yake yote, Mama Waitherero alijitokeza kama nanga ya familia ya Kibaki. Kama dada mkubwa wa Rais wa zamani Mwai Kibaki, alichukua nafasi kubwa katika kuunda maisha yake ya umma."

Rais Uhuru aliitakia familia ya Kibaki nguvu na faraja wanapomuomboleza marehemu Mama Waitherero.

"Namuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya mpendwa wetu Mama Esther Waitherero mahali pema peponi. Pia naomba Mungu aipe familia nzima ya Kibaki ujasiri wa kustahimili kifo cha mpendwa wao," Rais aliomba.

Marehemu alifariki akiwa na umri wa miaka 115.

Kifo cha Bi Waithera kimekuja takriban miezi mitatu baada ya kakake mdogo Mwai Kibaki kufariki. Kibaki aliaga mnamo Aprili 21 mwaka huu.