Wezi wa pesa wakamatwa na DCI wakiwa kwa mganga kutafuta zindiko ya kukwepa kukamatwa

Miriam Mwelu aliibia mwajiri wake shilingi milion 4 na mikufu kabla ya kutorokea kwa mganga ili kukwepa kukamatwa

Muhtasari

• DCI walisema mshukiwa wa wizi Miriam Mwelu aliiba pesa za mwajiri wake na kupelekwa na mumewe kwa mganga kwa zindiko.

• DCI walimkamata na akawapeleka kwa wazazi wake ambako milioni 1.57 zilipatikana.

Miriam Mwelu aliiba pesa za mwajiri wake na kushirikiana na mpenzi wake Timothy Akoi kutafuta huduma za mganga ili kukwepa kushikwa
Miriam Mwelu aliiba pesa za mwajiri wake na kushirikiana na mpenzi wake Timothy Akoi kutafuta huduma za mganga ili kukwepa kushikwa
Image: Facebook///DCI

Wapenzi wawili ambao pia wanashirikiana katika vitendo vya wizi jana walipatikana katika nyumba ya mganga wakitafuta zindiko ili kukwepa mkono wa makachero wa kitengo cha DCI ambao walikuwa wakiwasaka kwa muda mrefu baada ya kusemekana kuiba kiasi cha shilingi milioni 4 wiki tatu zilizopita.

Kulingana na taarifa kutoka wa wapelelezi wa DCI, Miriam Mwelu na mpenzi wake Timothy Akoi walishirikiana kumuibia mwajiri wa Miriam milioni 4 wiki tatu zilizopita na baada ya kusikia kwamba walikuwa wanasakwa na makachero wa DCI, waliamua kutafuta zindiko kwa mganga ili kukwepa kukamatwa.

DCI waliwavamia wawili hao kwenye nyumba ya mganga katika eneo la Gachie kaunti ya Kiambu ambako Mwelu alikuwa ameenda kuzindikwa ili kuwapotezea dira wapelelezi wa DCI.

"Wapelelezi wa DCI walifika kwa muda mwafaka na kumpata mtuhumiwa ndio anaingizwa kwenye beseni yenye vitu vya kishirikina vilivyosheheni damu ambayo ilitolewa kwa bundi aliyekufa ambaye muonekano wake unafanana ule wa jogoo," DCI walisema.

Inaarifiwa kwamab mzee huyo mganga baada ya kuwaona makachero wa DCI, alianza kutamka maneno yasiyoeleweka kama njiqa moja ya kulaani uvamizi wao katika maeneo yake ya kazi lakini haya yalianguka kwa masikio ya kiziwi kwani makachero hawakuahirisha mpango wao wa kumtia nguvuni mshukiwa ambaye kwa muda mrefu wamekuwa wakimsaka

Makachero wa DCI walisema kwamab walipata orodha ya baadhi ya huduma za mganga huyo ambapo moja wa huduma hizo ilikuwa ni 'kutoshikwa na DCI' ambayo kiasi chake kilikuwa ni tozo ya shilingi elfu tano pesa za Kenya.

Mwelu aliwaelekeza maafisa wa DCI mpaka nyumbani kwa wazazi wake kwenye kaunti ya Murang'a ambako shilingi milioni 1.57 zilipatikana pamoja na ushanga ghali qambao aliiba kutoka kwa mwajiri wake.