"Unachapa mtoto kwa kutofikisha alama 400, wewe ukitahiniwa utafikisha?" - Waziri Magoha

Waziri Magoha alikemea kitendo cha mwanafunzi wa darasa la nane wa shule ya Nyamninia aliyecharazwa vibaya.

Muhtasari

"• Kama mimi kama Waziri siwezi chapa mtoto, unadhani wewe ni nani kama mwalimu wa kawaida tu kuchapa mtoto wa watu namna ile?” - Waziri Magoha

Baada ya video kuvuja mitandaoni ikimuonyesha mtoto mmoja kutoka shule ya msingi ya Nyamninia huko Siaya akielezea na hata kuonesha jinsi ambavyo walimu walichapa viboko kwa kukosa kufikisha alama mia nne, sasa Waziri wa elimu profesa George Magoha amejitokeza wazi na kukemea kitendo hicho dhidi ya watoto.

Mtoto huyo ambaye ni mtahiniwa wa darasa la nane alielezea kwa uchungu na maumivu makali kwamba walimu walicharaza vikali kama mbwa koko aliyepakitana msikitini kisa tu kutofikisha alama mia nne katika mtihani wa mwigo waliofanya shuleni humo.

Waziri Magoha sasa amesisitiza kwamab kitendo hicho ni cha unyama na walimu wanaokitekeleza pengine hawakufikisha alama kama hizo wanazolazimisha mtoto kupata, enzi zao wakiwa shule za msingi.

“Ni kinyume cha sheria kuchapa watoto shuleni, kama ambavyo sheria inasema mpaka sasa. Hata maoni yangu pia ni hivyo kwamba ni unyama kuchapa mtoto kama ambavyo unachapa mnyama. Na mtu yeyote amefanya masomo ya kufunza au utaalamu atakwambia kwamba kama mtoto amefanya wastani na unataka afanye vizuri zaidi, kuchapa huyo mtoto si kwamba umemsaidia aende kufanya vizuri kwenye mitihani,” Waziri Magoha alisema.

Waziri Magoha alisema kitendo kama hicho ni kumfanya mtoto ajenge uadui na walimu na hata kuogopa kutafuta msaada katika somo ambalo linamkalia gumu kwani atakuwa anawaona walimu kama maadui.

“Walimu wale haijalishi idadi yao mimi nafikiri tume ya kusimamia walimu ya TSC itawashughulikia vilivyo na nyinyi polisi hapa mna kazi ya kufanya ili kuhakikisha wanashtakiwa inavyofaa. Kila mtoto nchini Kenya ni wa umuhimu na hili liwe kama onyo kwa mtu yeyote, kama mimi kama Waziri siwezi chapa mtoto, unadhani wewe ni nani kama mwalimu wa kawaida tu kuchapa mtoto wa watu namna ile?” Waziri Magoha alifoka kwa hasira.

“Unachapa mtoto ati unataka afikishe alama 400, wewe mwenyewe unaweza fikisha alama hizo kama utatahiniwa katika kiwango kama hicho?” Magoha alipandwa na mori.

Sheria ya sasa nchini Kenya inaharamisha kuchapwa kwa wanafunzi shuleni na hilo kwa muda mrefu limekuwa gumzo haswa kipindi ambacho visa vya utovu wa nidhani shuleni vilizidi na wanafunzi wakawa wanateketeza mabweni.