Gavana Nyong'o aahidi kuendelea na ajenda ya maendeleo

Muhtasari
  • Kisumu ina wapigakura 606,754 waliojiandikisha
  • Mudanya aliwasilisha cheti hicho kwa Nyong’o
  • Alimpongeza Mudanya na timu kwa kufanya uchaguzi wa kuaminika
  • Nyong'o aliahidi kuendelea na ajenda yake ya maendeleo
Magavana James Ongwae (Kisii), Anyang' Nyong'o (Kisumu) na Abdi Mohamud (Wajir) wakihutubia wanahabari nje ya afisi za Baraza la Magavana huko Oracle, Westlands, Aprili 1. Picha: MAKTABA
Magavana James Ongwae (Kisii), Anyang' Nyong'o (Kisumu) na Abdi Mohamud (Wajir) wakihutubia wanahabari nje ya afisi za Baraza la Magavana huko Oracle, Westlands, Aprili 1. Picha: MAKTABA
Image: MAKTABA

Gavana wa Kisumu Anyang' Nyong’o na naibu gavana Mathews Owili wamechaguliwa tena kwa muhula wa pili.

Nyong’o alipata kura 319,957.

Gavana wa zamani Jack Ranguma aliibuka wa pili kwa kura 100,600.

Ranguma alikuwa ameungana na Seneta anayeondoka Fred Outa, aliyekuwa spika wa Kisumu Onyango Oloo na aliyekuwa Mbunge wa Kisumu ya Kati Ken Obura katika azma yake ya kumng'oa Nyong'o.

Nyong’o alitetea kiti hicho kwa tiketi ya ODM, huku Ranguma akiwania kwa tikiti ya MDG. Kinyang'anyiro hicho kilivutia wagombea wanne.

Beryl Meso, mgombeaji wa kujitegemea alipata kura 3,383, huku Erick Otieno akipata kura 2,705.

Msimamizi wa uchaguzi wa IEBC katika kaunti hiyo Solomon Mudanya alitangaza matokeo hayo katika kituo cha kujumlisha matokeo cha Chuo cha Tom Mboya Labour siku ya Ijumaa.

Kisumu ina wapigakura 606,754 waliojiandikisha.

Mudanya aliwasilisha cheti hicho kwa Nyong’o.

Alimpongeza Mudanya na timu kwa kufanya uchaguzi wa kuaminika.

Nyong'o aliahidi kuendelea na ajenda yake ya maendeleo.

Alitoa mfano wa afya, elimu, mazingira, kilimo na uendelevu wa maisha kwa sababu yanahusu mahitaji muhimu ya wananchi.

Nyong’o aliwapongeza wakazi wa Kisumu kwa kumpigia kura kuhudumu kwa muhula mwingine.

"Tuko tayari kuhakikisha tunatekeleza ahadi zetu za uchaguzi kuhusu masuala ya maendeleo," alisema.

Pia amempongeza Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa maendeleo ya haraka waliyofanya katika Bandari ya Kisumu, ambayo alisema yatabuni nafasi za kazi na biashara kwa wananchi.