• Shule zilifungwa wiki jana ili kupisha tume ya IEBC kutumia baadhi ya shule kama vituo vya kupiga kura.
Waziri wa elimu msomi George Magoha kwa mara nyingine tena ameendelea kuwachanganya wazazi na washikadau katika sekta ya elimu baada ya kutangaza tarehe mpya za kufunguliwa kwa shule kufuatia kufungwa wiki jana ili kupisha tume ya IEBC kutumia baadhi ya shule hizo kama vituo vya upigaji kura.
Awali, Magoha alikuwa ametangaza kwamba shule zingefunguliwa tarehe 11 Agosti, siku tatu tu baada ya kukamilika kwa mchakato wa kupiga kura.
Hata hivyo, siku mbili zilizopita, Waziri huyo tena alitangaza upya kwamba kufuatia shughuli pevu ya kuhesabu kwa kura ambayo inaendelea katika baadhi ya vituo, shule zingefunguliwa Agosti 15 ambayo ni Jumatatu wiki kesho, na kuwataka wazazi wote kujipanga kuwarudisha watoto shuleni.
Hata hivyo, huu si uamuzi wa mwisho kwani Jumamosi tena Waziri Magoha amezuka na taarifa mpya huku akisema kwamba tarehe ya kufunguliwa kwa shule imesogezwa mbele hadi tarehe 18 Agosti ambayo ni Alhamis wiki kesho.
“Kufuatia upigaji kura uliofanyika Jumanne, mchakato wa kuhesabu kura hizo ungali unaendelea na hivyo baada ya mashauriano ya muda, sasa ninatoa agizo la serikali la kuzitaka shule ziendelee kufungwa kwanzia Jumatatu na kufunguliwa Alhamis badala yake kwa ajili ya masomo ya kawaida. Taarifa hizi zinafunika taarifa za awali zilizotaka shule kufunguliwa Agosti 15,” taarifa kwa vyombo vya habari ilisoma.