"Nawaomba tuvumiliane tusaidie wanafunzi" Magoha awasihi walimu wakuu

Waziri huyo aliwaomba walimu kutowafukuza karo wanafunzi ambao hawajakamilisha malipo hayo

Muhtasari

• Amewashukuru walimu na wazazi ambao wamejikaza kuhakikisha wanafunzi wako shuleni licha ya hali ngumu ya maisha na misukosuko ya kufunga shule kabla na hata baada ya uchaguzi.

Waziri wa Elimu George Magoha katika shule moja eneo la Kabete Nairobi
Waziri wa Elimu George Magoha katika shule moja eneo la Kabete Nairobi
Image: HISANI

Waziri wa elimu Prof George Magoha amewataka walimu wakuu kuwaruhusu wanafunzi kubakia shuleni hata kama hawajakamilisha karo.

Akizungumza katika shule ya upili ya Mary Leaky iliyoko katika eneo bunge la Kabete, kaunti ya Nairobi ambapo alikuwa akifungua rasmi madarasa ya mtaala wa usalimi na utendaji[CBC], Mahoga alisisitiza umuhimu wa wanafunzi ambao muda wao wa masomo ulikatizwa ili kuruhusu kura kuu za uchaguzi kufanyika.

“Naomba walimu wakuu msiwatume wanafunzi nyumbani kwa sababu ya karo. Mungu amekubali wao kurudi salama. Ikiwa kuna tatizo, suluhisha na mzazi au wizara,” Alisema Waziri Magoha.

Aidha ameeleza haja ya kuboresha miundomisingi zaidi ili kutosheleza idadi kubwa ya wanafunzi. Amesema kuwa ugavi wa kufadhili masomo ya wanafunzi wasiojiweza kutoka kwa serikali utaanza kupokewa kwanzia wiki ijao.

“Najua tatizo linalowakumba walimu katika kuendeleza shughuli shuleni wakati hamna pesa. Ninawaakikishia kwamba serikali imetoa pesa na ziko tayari,hivyo kuanzia wiki ijao shule zitaanza kupokea,” Alisema.

Waziri amesema mradi huo utakuwa wa miaka minee kwa kila mwanafunzi wala si mwaka mmoja kama ilivyokuwa awali.

Amewashukuru walimu na wazazi ambao wamejikaza kuhakikisha wanafunzi wako shuleni licha ya hali ngumu ya maisha na misukosuko ya kufunga shule kabla na hata baada ya uchaguzi.