Afueni kwa 'comrades' mahakama ikiharamisha HELB kutoza riba na faini zinazozidi kiwangi cha msingi

Mshtakiwa (HELB) anakiuka Ibara ya 43 (1) (e) na (f) na Ibara ya 27 ya Katiba. ya Kenya - Jaji Alfred Mabeya

Muhtasari

• Mahakama moja jijini Nairobi imeamuru kwamba ni hatia kwa bodi ya HELB kutoza riba na faini zinazozidi kiwango cha msingi ambacho iliwapatia wanufaika

Wahitimu wa chuo kikuu
Mahafali Wahitimu wa chuo kikuu
Image: THE STAR

Ni afueni kwa watu waliokuwa wanufaika wa mkopo wa elimu ya juu HELB baada ya mahakama moja jijini Nairobi kuamuru kwamba ni hatia kwa bodi ya HELB kutoza riba na faini zinazozidi kiwango cha msingi ambacho iliwapatia wanufaika hao kipindi wakiwa wanafunzi vyuoni.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa katika jarida moja la humu nchini, jaji Alfred Mabeya wa mahakama kuu alitoa uamuzi na kuwaunga mkono wanufaika watatu ambao walielekea mahakamani kupinga hatua ya bodi ya HELB kutoza viwango vya riba na faini vinavyozidi kiwango cha msingi ambacho walinufaika kutoka kwao wakiwa vyuoni. Walalamishi hao ambao walikuwa wanufaika wa HELB ni pamoja na Ann Mugure, Davis Nguthu na Wangui Wachira ambao waliteta vikali kuhusu riba na faini za juu zinazolimbikiziwa watu ambao waliwahi kunufaika na mkopo huo wa elimu ya juu, jambo lililowapelekea kuunganisha nguvu zao na kutafuta haki mahakamani.

“Tamko hili linatoa tamko dhidi ya mlalamikiwa (Helb) kwamba kwa kuweka viwango vya riba na adhabu au faini zinazozidi kiwango cha msingi, mlalamikiwa anakiuka Ibara ya 43 (1) (e) na (f) na Ibara ya 27 ya Katiba. ya Kenya,” jarida hilo lilimnukuu Jaji Mabeya katika hukumu hiyo.

Kulingana na hati zilizowasilishwa kortini, watatu hao kwa tarehe tofauti walikopa mikopo kutoka kwa Helb ili kuwezesha masomo yao ya shahada ya kwanza, lakini riba kubwa na adhabu zilifanya uwezo wao wa kulipa kuwa mgumu.

Waombaji hao walibaini kuwa mnamo Novemba 2020 kupitia ukurasa wake wa Twitter, Helb ilitishia kuchapisha majina na picha hizo kwenye magazeti maarufu ya waliokiuka sheria na kutoa notisi ya siku 30 ya ulipaji.

Takwimu za hivi punde kutoka Helb zinaonyesha kuwa mikopo ambayo haijalipwa na watu waliokuwa wanufaika kwa vipindi tofauti ni zaidi ya bilioni 10.2 pesa za benki kuu ya Kenya ambapo bodi hiyo imekuwa ikiwarai wanufaika kufanya hima kulips mikopo hiyo ili kuwawezesha wengine ambao wanajiunga vyuo vikuu pia kunufaika na kufanya muendelezo wa masomo yao ya vyuoni kuwa rahisi.