Mwanaume achoma nyumba na kujichimbia kaburi baada ya kushindwa kulipa mkopo

Mwanaume huyo alisemekana kuwa mwalimu kabla ya janga la Korona.

Muhtasari

• Alizidiwa na mzongo wa mawazo baada ya wenye mkopo kuchukua sehemu ya shamba lake alilokuwa ameliweka kama dhamana.

Nyumba iliyochomwa
Nyumba iliyochomwa
Image: maktaba

Mwanaume mmoja katika kaunti ya Kisii amezua kioja baada ya kuchoma nyumba za boma lake na kujichimbia kaburi alilodai kwamba litatumika kumzika yeye pindi atakapofariki.

Kulingana na taarifa katika wavuti wa kituo kimoja humu nchini, familia hiyo iliyopo eneo bunge la Nyaribari Masaba Kijiji cha Ibacho sasa italazimika kushinda nje bila makazi baada ya nyumba zote kuchomwa moto na baba wa boma hilo.

Inaarifiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa na msongo wa mawazo kutokana na mkopo aliouchukua ili kuitia familia yake nakshi baada ya janga la Korona kudhoofisha mapato yao na aliposhindwa kustahimili shinikizo kutoka kwa wenye mkopo, alichukua uamuzi wa kutia nyumba zake moto kabla ya kufanya jaribio la kukatisha maisha yake pia ambapo tayari alikuwa amechimba kaburi la kuizika maiti yake.

Msongo wa mawazo ulizidi hata zaidi baada ya sehemu ya ardhi yake kuchukuliwa kama fidia ya mkopo huo, jambo lililomsukuma mzee huyo kuwa mtiribu wa kila aina ya kileo kaam njia moja ya kujifariji mbali na unyongovu uliokuwa ukimkodolea macho, lakini unaambiwa dhiki ikizidi piam huonekana nyanda, kwake mzee huyu, nyanda ilikuwa katika paji la uso wake ambapo alishindwa kuhimili kabisa.

Mwanaume huyo alisemekana kuwa mwlimu kabla ya janga la Korona kubisha na walichukuwa mkopo ili kuanzisha mradi wa kujenga madarasa ya kuanzisha shule la kibinafsi sehemu hiyo ila mipango yote ikabuma na mkopo wenyewe walikuwa wameweka hatimiliki ya shamba lao kama dhamana.

Kilichosikitisha wakaazi ni kwamba mwanaume huyo alichimba kaburi lake katika moja ya nyumba hizo kabla ya kuziteketeza, ila kwa bahati nzuri hakufanikiwa kujiua kama alivyokusudia kwani vyombo vya dola viliwahi kwa muda na kumtia nguvuni ambapo alipelekwa katika kituo cha polisi eneo hilo akisubiria kufikishwa mahakamani kwa shtaka la kuharibu mali na kutishia maisha.