Kama korti itaamua turudie kura,Chebukati anapaswa kujiuzulu-Mbunge Kimilu

Kimilu pia alisema Makamishna wanapaswa pia kujiuzulu, akiongeza kuwa bodi ya uchaguzi inapaswa kuongozwa na watu wanaokumbatia haki na uadilifu.

Muhtasari
  • "Tunahimiza mahakama zetu kuhakikisha kwamba hazikatizwi na mtu wa nje. Waache wafanye kazi yao," alisema.

Mbunge wa Kaiti Joshua Kimilu sasa anamtaka mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kujiuzulu.

Kimilu alidai kuwa Chebukati ndiye chanzo cha mizozo ya uchaguzi wa 2022 na kuongeza kuwa ikiwa Mahakama ya Juu itatangaza uchaguzi urudiwe, Chebukati hafai kuwa msimamizi wa uchaguzi huo.

"Kama koti itaamua turudie kura, tunasema ya kwamba hatutakubali Chebukati hapo. Aende nyumbani," Alisema Kimilu.

Kimilu pia alisema Makamishna wanapaswa pia kujiuzulu, akiongeza kuwa bodi ya uchaguzi inapaswa kuongozwa na watu wanaokumbatia haki na uadilifu.

“Hata ikichukua mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa marudio hayo ni sawa, ilimradi tutakuwa na mtu ambaye anaweza kuleta haki katika nchi yetu,” alisema.

Mbunge huyo wa chama cha Wiper alisema watakubali uamuzi wa Mahakama.

"Tunahimiza mahakama zetu kuhakikisha kwamba hazikatizwi na mtu wa nje. Waache wafanye kazi yao," alisema.

Kimilu aliongeza, "Kwa upande wetu tuko tayari kukubali hukumu hiyo. Tunajua Azimio atashinda... Tunajua ushahidi tuliowasilisha utatosha na haki itatendeka."