Milioni 200 zatengwa kwa ajili ya kuapishwa kwa Ruto

Hafla hiyo inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo, Septemba 13.

Muhtasari

•Fedha hizo zimetengewa Kamati ya Kukabidhiwa Ofisi ambayo kwa sasa inajiandaa kwa mpito wa mamlaka.

•Mnamo Jumatatu, timu ya maafisa wa serikali ilikagua uwanja wa Kasarani.

RAIS MTEULE WILLIAM RUTO
Image: ANDREW KASUKU

Itagharimu hazina ya kitaifa shilingi milioni 200 kuandaa hafla ya kuapishwa kwa Rais mteule William Ruto.

Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya kiuchumi ya Hazina kabla ya Uchaguzi Mkuu.

"Shilingi milioni 200 zimetolewa katika bajeti ya kipindi cha mwaka  2022-2023 kutekeleza shughuli za uhamisho wa mamlaka  kutoka serikali inayoondoka hadi serikali mpya ," inasoma ripoti hiyo.

Fedha hizo zimetengewa Kamati ya mpito ambayo kwa sasa inajiandaa kwa mpito wa mamlaka kutoka kwa Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta hadi William Ruto.

Hafla hiyo inayotarajiwa kufanyika wiki ijayo, Septemba 13 (Jumanne) itashuhudia Ruto na naibu wake mteule Rigathi Gachagua wakiapishwa kuwa rais.

Kulingana na Sura ya 141 ya Katiba ya Kenya, tukio hilo limepangwa kufanyika Jumanne ya kwanza, siku saba baada ya tarehe ambayo Mahakama ya Upeo inatoa uamuzi wa kutangaza uchaguzi kuwa halali.

Kisha Rais mteule anachukua madaraka kwa kula kiapo cha utii na kuapa kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake.

Sheria ya Kuchukua Ofisi ya Rais inaunda kamati itakayohusika na usimamizi wa tukio la kuapishwa na kutoa taarifa za usalama kwa rais ajaye.

Ratiba yao ya shughuli ilianza mara tu baada ya mahakama kumtangaza Ruto kuwa Rais mteule, hali hiyo hiyo ikiwa imesimamishwa kabla ya uamuzi huo.

Kamati hiyo, kwa mujibu wa sheria, inatarajiwa kuchapisha, kwa notisi kwenye Gazeti la Kenya, tarehe na mahali pa kuapishwa, ambayo lazima iwe ndani ya Nairobi.

Mnamo Jumatatu, timu ya maafisa wa serikali ilikagua uwanja wa Kasarani.

Ruto alikuwa amewateua Spika wa Bunge la Kitaifa anayeondoka Justin Muturi, Katibu Mkuu wa UDA Veronica Maina na Mbunge wa Uasin Gishu Gladys Shollei kuwa wanachama walioteuliwa katika timu inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua.

"Kuapishwa kwa Rais Mteule kutafanywa katika hafla ya hadhara itakayofanyika katika mji mkuu," sheria inasema, na kuongeza kuwa siku hiyo itakuwa sikukuu ya umma.

Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi ataapisha rais mteule mbele ya Jaji Mkuu Martha Koome au Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu akiwa hayupo. 

Kiapo lazima kifanyike kabla ya saa nane mchana, huku sheria ikieleza kwamba Naibu Jaji Mkuu ndiye pekee anayeshughulikia jukumu hilo pale ambapo Jaji Mkuu hana uwezo. 

Ruto atahitajika kutia sahihi cheti cha kuapishwa mbele ya Jaji Mkuu au Naibu Jaji Mkuu. 

Baada ya kutiwa saini, Rais Uhuru Kenyatta atakabidhi upanga na Katiba kwa Ruto kuashiria kukabidhiwa mamlaka. 

Ruto atakuwa wa kwanza kula kiapo kabla ya naibu wake, Rigathi Gachagua, kuanza kula kiapo hicho, huku kukiwa na marekebisho kidogo ili kuendana na majukumu ya ofisi yake. 

"Rais, baada ya kuapishwa kwa Naibu Rais mteule, atatoa hotuba ya kuapishwa kwa taifa," sheria inasema.