Amason Kingi achaguliwa Spika wa Seneti kwa kura 46

Shughuli ya upigaji kura na kuapishwa kwa Kingi iliyongozwa na katibu wa seneti Jeremiah Nyegenye.

Muhtasari

• Kingi alichaguliwa katika awamu ya kwanza kwa kuafikia kigezo cha thulithi mbili ya idadi ya maseneta.

Spika mpya wa seneti Amason Kingi akihutubia maseneta muda mfupi baada ya kuapishwa
Spika mpya wa seneti Amason Kingi akihutubia maseneta muda mfupi baada ya kuapishwa

Aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi ndiye spika wa seneti baada ya kuzoa jumla ya kura 46.

Kingi alichaguliwa katika awamu ya kwanza kwa kuafikia kigezo cha thulithi mbili ya idadi ya maseneta.

Kuna jumla ya maseneta 67 wakiwemo walioteuliwa na thulithi mbili ni maseneta 45.

Awali uwezekano wa Kingi kuchaguliwa ilipigwa jeki kufuatia kujiondoa kwa mgombea wa muungano wa Azimio Kalonzo Musyoka.

Kingi sasa anachukuwa nafasi ya Ken Lusaka ambaye ni gavana wa Bungoma.

Shughuli ya upigaji kura na kuapishwa kwa Kingi iliyongozwa na katibu wa seneti Jeremiah Nyegenye. 

Mapema muungano wa Azimio ulipata pigo baada ya mgombea wake Kalonzo Musyoka kujiondoa kutoka kinyang’anyiro hicho.

Hatua hiyo ya Kalonzo ilitangazwa na katibu wa Seneti Jeremiah Nyegenye.

Nyegenye alisema kwamba ofisi yake ilikuwa imepokea barua asubuhi siku ya Alhamisi kutoka kwa Kalonzo akiondoa azma yake.

Maseneta katika muungano wa Azimio siku ya Jumatano walikuwa wameafikia kwa kauli moja kumuunga mkono Kalonzo kwa wadhifa wa Spika wa seneti.

Mapema Jumahili Kalonzo alikuwa amechukuwa stabadhi kuania wadhifa wa spika katika bunge na Seneti lakini akabadili mawazo na kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa bunge la Kitafia ili awanie nafasi ya spika wa seneti.

Bado haijabainika sababu kuu ya Kalonzo kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha spika wa seneti.