Ruto asikitika kuwa Uhuru hajapongeza ushindi wake

Rais mteule ashikilia kuwa "hakuna nafasi" ya ushoga katika jamii ya Kenya

Muhtasari

• Ruto alimshinda mpinzani wake wa karibu Raila Odinga wa Azimio kwa kura chache.

• Rais Uhuru Kenyatta akihutubia wabunge na maseneta waliochaguliwa chini ya mwavuli wa Azimio alisema kwamba kwake Raila bado ndiye atasalia kiongozi wake.

• Ruto, 55, alishinda kwa 50.49% ya kura dhidi ya 48.85% ya Odinga katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na rais mteule William Ruto
Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na rais mteule William Ruto

Rais mteule William Ruto ameelezea masikitiko yake kwamba tangu atangazwe mshindi wa uchaguzi wa Agosti 9, hajapongezwa na rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha CNN Jumatano usiku Ruto alisema kuwa huenda Uhuru alikasirishwa na kushindwa kwa mgombea ambaye Uhuru alikuwa akiunga mkono.

"Kwa bahati mbaya, Rais Kenyatta hajaona maana ya kunipongeza,..Labda amekata tamaa au hafurahii kwamba nilimshinda mgombea wake, lakini hiyo ndiyo asili ya siasa,"Ruto alisema.

Rais Uhuru Kenyatta akihutubia wabunge na maseneta waliochaguliwa chini ya mwavuli wa Azimio alisema kwamba kwake Raila bado ndiye atasalia kiongozi wake.

Uhuru hata hivyo alibainisha kwamba bila shaka atamkabidhi Ruto mamlaka kwa sababu ni jukumu lake kikatiba lakini Raila ndire kiongozi anayemtambua.

"Nitamkabidhi madaraka nikitabasamu kwa sababu ni jukumu langu Kikatiba kufanya hivyo, lakini kiongozi wangu ni Baba Raila Odinga," rais Kenyatta alisema.

Rais mteule William Ruto hata hivyo aliambia CNN kwamba atafanya juhudi kuunganisha taifa ambalo limegawanyika karibu nusu.

Ruto alimshinda mpinzani wake wa karibu Raila Odinga wa Azimio kwa kura chache.

 “Utawala nitakaosimamia utakuwa utawala ambao utahudumia Wakenya wote kwa usawa, iwe walitupigia kura au hawakutupigia kura,” alisema Ruto.

Ruto, 55, alishinda kwa 50.49% ya kura dhidi ya 48.85% ya Odinga katika uchaguzi wa mwezi uliopita.

Kuhusu uhusiano wa kimapenzi wa watu wa jinsia moja, rais mteule William Ruto alisema kwamba "hakuna nafasi" ya ushoga katika jamii ya Kenya. 

"Niko wazi kuwa tunaheshimu kila mtu na kile anachoamini, lakini pia tuna kile tunachoamini na tunatarajia kuheshimiwa kwa kile tunachoamini," alisema Ruto. 

Ruto alisema swala ushoga sio mada muhimu kwa Wakenya.Rais mteule vile vile alipuuzilia mbali madai kwamba ana njama ya kuwafurusha raia wote wa Uchina nchini Kenya.

 Alibainisha kwamba alikuwa akizungumzia Wachina wanaofanya kazi nchini bila kibali. 

"Kila mtu atafanya biashara, kila mtu atafanya anachotaka ili mradi anafanya kwa mujibu wa sheria," alisema. 

"Mtu yeyote anayefanya kazi nje ya sheria, haijalishi anatoka wapi, atarudishwa alikotoka."