Mwanadada afariki Saudi Arabia, familia yajulishwa kifo chake miezi 6 baadae

Mrembo huyo aliseekana kufariki mwezi mmoja tu kabla ya kufika Saudia, familia ilikuja kujulishwa miezi 6 baadae na kuambiwa mwili ungesafirishwa miezi miwili kutoka Agosti.

Muhtasari

• "Ninahangaika mchana na usiku na sikupata hiyo salamu kama mtoto wangu amekufa,” Mishi Khamis, mamake marehemu.

• Alisema kila walipojaribu kumfikia ajenti, alikuwa anawachezesha karata ya pata potea.

Mwanakombo Bahmad mrembo aliyefariki Saudia
Mwanakombo Bahmad mrembo aliyefariki Saudia
Image: Screengrab//Twitter

Familia moja katika kaunti ya Mombasa inazidi kulilia haki baada ya mpendwa wao kusemekana kufariki katika taifa la Saudi Arabia mwezi mmoja tu baada ya kutua katika taifa hilo la Uarabuni.

Kutilia msumari moto kwenye kidonda, familia hiyo inasema kwamab mwanao alifariki mwezi Februari mwaka huu ila wamekuja kujulishwa juzi mwezi Agosti, miezi sita baadae na wanaambiwa kwamab mwili huo wa mwanao utasafirishwa nchini baada ya miezi miwili ijayo, kufanya jumla ya miezi 8 tangu kifo chake kutokea kwa njia zisizoeleweka.

Katika ripoti ya kituo kimoja cha runinga humu nchini, Mwanakombo Bahmad mweney umri wa miaka 23 alisafiri kutoka nchini Januari mwaka huu na ghafla mawasiliano yakapotea baina yake na familia yake.

Mamake aliambia runinga hiyo kwamba alikuja kufahamishwa miezi sita baadae kwamab mtoto wake alishafariki kitambo.

“Ni juzi hiyo mwezi wa nane tarehe kumi na nne ndio Napata hizo habari, na Mwanakombo alifariki tangu mwezi wa pili tarehe tano. Sasa nikashangaa kwa nini hawakunielezea kutoka hizo siku, hiyo ndio uchungu ambayo ninahisi. Ninahangaika mchana na usiku na sikupata hiyo salamu kama mtoto wangu amekufa,” Mishi Khamis aliambia ripota baina ya majonzi na uchungu mkali wa mama kumpoteza mwana.

Kulingana na familia hiyo, baada ya kumjulisha ajenti aliyemsafirisha mwanao Kwenda Saudi Arabia aliwapa kisogo hata baada ya kumtaarifu kwamab mwanao anasema anateswa.

“Kila nilipokuwa nikimpigia ajenti simu, alikuwa ananiambia kwamba Mwanakombo alitoroka,” alieleza.

Taarifa hizi zinakuja siku chache tu baada ya mwanadada mmoja Diana Chepkemoi kuokolewa kutoka Saudia alipokuwa akifanya kazi na kuonekana kudhoofika kiafya mno.

Picha za kina dada waliokwenda Saudia kufanay kazi za ndani zikiwaonyesha katika hali mbaya ya kiafya zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii huku Wakenya wakizua vikali mtandaoni kuhusu ukimya wa serikali na ubalozi wake katika taifa hilo la jangwani Mashariki ya Kati.