Mwanaume apigwa risasi na kufa akijaribu kumuokoa mpenziwe kutoka kwa majambazi

Geoffrey Sigei walikuwa wamerejea nyumbani na mpenzi wake Winfred Kairuthi kwa magari tofauti asubuhi ya 4:30am

Muhtasari

• Kulingana na mlinzi wa ghorofa hiyo Samuel Wafula, Winfred alikuwa wa kwanza kuingia langoni akifuatwa na marehemu,

Picha ya bastola aina ya Ceska
Picha ya bastola aina ya Ceska
Image: MUSEMBI NZENGU

Mwanaume mmoja amefariki kwa kumiminiwa risasi na majambazi waliomteka mpenzi wake.

Kitengo cha upelelezi wa jinai wameripoti kwamba mwanaume huyo kwa jina Geoffrey Sigei alikuwa anajaribu kumuokoa mpenzi wake kwa jina Winfred Kairuthi aliyevamiwa na genge la wezi.

Katika tukio hilo lililoripotiwa kufanyika Jumapili asubuhi, wapenzi hao wawili walirejea nyumbani katika eneo la Ruiru Kiambu kila mmoja akiliendesha gari lake. Mwanadada ndiye alikuwa wa kwanza kushuka na kuvamiwa na majambazi hao ambapo mpenzi wake Sigei aliona hali hilo na kujaribu kukimbia kumnusuru ila mtutu wa bunduki ukageuzwa katika kifua chake.

“Marehemu Geoffrey Sigei na mpenzi wake Winfred Kairuthi, 34, walikuwa wamefika katika ghorofa hiyo kwa magari mawili tofauti mwendo wa saa 4:30 asubuhi, walipokabiliwa na majambazi wenye silaha. Kulingana na mlinzi wa ghorofa hiyo Samuel Wafula, Winfred alikuwa wa kwanza kuingia langoni akifuatwa na marehemu,” DCI waliripoti.

“Baada ya magari hayo kupita lango kuu, wanaume watatu waliingia ndani kwa nguvu, wakaenda moja kwa moja kwenye gari la Winfred na kuanza kulivamia. Marehemu alipokuwa akiegesha gari lake, aliwaona majambazi hao wakikabiliana na Winfred na kwenda kumsaidia huku wakiwa na rungu,” Mlinzi Wafula alirekodi taarifa.

Baada ya kuzua, majambazi hao waliokuwa wamejihami kwa bunduki walimfyatulia risasi na kutoweka. Majirani walioshtushwa na milio ya risasi walifika katika eneo hilo na kumkimbiza Sigei katika hospitali ya rufaa ila akaaga dunia kutokana na kuvuja damu kwa wingi.

Polisi walisema kwamba walikusanya taarifa majambazi hao walikuwa wakiwafuata wapenzi hao wawili kwa gari zito aina ya Toyota Prado TX wawili hao wakirejea nyumbani baada ya usiku wa tafrija katika sehemu moja ya starehe.