Kijiti nilipokezwa na Kibaki sikukitupa, namkabidhi Ruto - Hotuba ya mwisho ya Kenyatta

Kuapishwa ndio hatua ya mwisho katika mchakato wa kipindi cha uchaguzi

Muhtasari

• "Ni wakati wa kukusanyika pamoja kama watu wamoja, kutekeleza ahadi ya Kenya, kama ilivyokusudiwa na Mungu" - Kenyatta.

Rais uhuru kenyatta akisalimiana na rais mteule William Ruto
Rais uhuru kenyatta akisalimiana na rais mteule William Ruto
Image: PSCU

Baada ya minong’ono na wasi wasi mwingi haswa kweney mitandao ya kijamii kuhusu ukimya wa rais anayeondoka Uhuru Kenyatta kutompongeza wazi wazi rais ajaye William Ruto katika hotuba yake ya awali, jana hatimaye rais Kenyatta alimeza yote na kutoa pongezi zake kwa rais Ruto.

Katika hotuba yake ya mwisho iliyojawa na hisia mseto, rais Kenyatta alizungumzia mengi na kusisitiza kwamba yeye katika nafasi yake kama rais anayeondoka, atashiriki kwa kikamilifu shughuli ya kuapishwa kwa rais mpya na kumkabidhi madaraka kulingana na takwa la katiba ya mwaka 2010 ya Kenya.

Katika kipengee kimoja cha hotuba yake, rais Kenyatta alisema kwamba kulingana na katiba, shughuli ya kuapishwa kwa rais mpya ndio mchakato wa mwisho kabisa kuhitimisha shughuli ya uchaguzi.

Alisema yeye kijiti alichopokezwa na hayati rais wa tatu Mzee Mwai Kibaki hakukiangusha chini bali katika wakati wake mbioni, alijenga historia kubwa ya maendeleo ambayo haitokuja kukaa ikasahaulika na kusema kijiti hicho pia atamkabidhi rais mpya William Ruto ili kuendeleza mbio za kuisogeza Kenya kwenye ngazi zingine kimaendeleo na kidemokrasia pia.

“Kuapishwa ndio hatua ya mwisho katika mchakato wa kipindi cha uchaguzi, ni wakati wa kukusanyika pamoja kama watu wamoja, kutekeleza ahadi ya Kenya, kama ilivyokusudiwa na Mungu. Fimbo tuliyopokea kutoka kwa marehemu rais Mwai Kibaki haikutupwa. Tulijenga juu ya urithi wake,” rais Kenyatta alisema.

Kenyatta alichukua nafasi hiyo pia kumpongeza mrithi wake William Ruto na kumtakia kila la kheri katika safari yake kuchukua hatamu kama rais wa tano wa Kenya.

Rais uhuru kenyatta akisalimiana na rais mteule William Ruto
Rais uhuru kenyatta akisalimiana na rais mteule William Ruto
Image: PSCU