Ruto atoa amri ya kwanza kama rais "Kurudishwa kwa bandari ya Mombasa"

Hii itarejesha maelfu ya kazi kwa wakazi wa Mombasa - Ruto.

Muhtasari

• Vile vile rais huyo mpya alitangaza jioni hii pia atawateuwa majaji waliopendekezwa na idara ya mahakama ila rais mstaafu Uhuru Kenyatta akawachuja.

Rais Ruto atoa amri yake ya kwanza kama rais
Rais Ruto atoa amri yake ya kwanza kama rais
Image: Facebook

Saa chache tu baada ya kutangazwa kama rais wa tano wa Kenya, William Ruto katika kile ameonekana kuanza kazi kwa kasi ya ajabu, tayari ametoa amri ya kurudishwa kwa shughuli za bandari ya Mombasa.

Agizo hili ambalo alisema amelitoa na leo jioni atatoa habari zaidi jinsi mchakato huo utafanyika linaonekana kama ni kuanza kutimiza ahadi zake haswa kwa watu wa Pwani ya Kenya kipindi cha kampeni zake ambapo si mara moja alisikika akiahidi kwamba uongozi wake utarejesha shughuli za bandari ya Mombasa.

Katika hotuba yake ya kwanza kama rais, Ruto alizungumzia mambo mengi na kusisitiza kwamba mengine yanaanza jioni hii, hilo la Bandari likiwa mojawapo ambalo atalishughulikia pindi atakapoingia kweney ofisi ya rais baada ya kumalizika kwa hafla ya kuapishwa kwake katika uga wa Kasarani.

“Jioni ya leo nitatoa maagizo ya kuidhinishwa kwa bidhaa ili kurejea katika bandari ya Mombasa nilivyotoa ahadi. Hii itarejesha maelfu ya kazi kwa wakazi wa Mombasa,” Ruto alisema.

Vile vile rais huyo mpya alitangaza jioni hii pia atawateuwa majaji waliopendekezwa na idara ya mahakama ila rais mstaafu Uhuru Kenyatta akawachuja.

Ruto alisema Kesho Septemba 14 atasimamia mchakato wa kuapishwa kwa majaji hao ili kuanza kuhudumu mara moja.

Hapa kazi mwendo kasi tu!