Tuko tayari kama KRA kufanya kila tuwezalo kuunga mkono serikali ya Ruto - Githii Mburu

Githii Mburu ni kamishna jenerali wa mamlaka ya ukusanyaji tozo nchini KRA

Muhtasari

• Tumejitolea kukusanya mapato yote yanayopatikana ndani ya uchumi wetu ili kusaidia ajenda yetu ya maendeleo - KRA.

KRA wamesema watafanya kazi kuhakikisha uongozi wa Ruto umefaulu.
KRA wamesema watafanya kazi kuhakikisha uongozi wa Ruto umefaulu.
Image: Maktaba, Facebook

Mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini KRA imeanza kazi rasmi chini ya uongozi mpya wa rais William Ruto.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, kamishna jenerali wa KRA Githii Mburu dakika chache tu baada ya rais Ruto kula kiapo, alisema kwamba mamlaka hiyo ipo tayari kuwafuata watu wote ili kuhakikisha wamelipa ushuru ili kuiwezesha serikali ya Ruto kuwahudumia wakenya.

Katika msururu wa Tweets, Mburu alisisitiza kwamba safari hii hakuna Mkenya atakayesazwa dhidi ya kulipa ushuru na kodi zote kwani serikali mpya itahitaji kufanikisha manifesto yake na ni kupitia kwa tozo ndio hilo litawezekana.

“Tuko tayari kama KRA kufanya kila tuwezalo kuunga mkono serikali hii ili kufikia matarajio ya Wakenya. Tumejitolea kukusanya mapato yote yanayopatikana ndani ya uchumi wetu ili kusaidia ajenda yetu ya maendeleo. Sote tunaweza kufanya vyema zaidi kusaidia nchi yetu ikiwa kila mtu atalipa anachodaiwa - si shilingi zaidi na si shillingi pungufu - tutafanya kile kinachohitajika kwetu kama Wakenya katika kuunga mkono nchi yetu,” Githii Mburu alisema.

Matamshi haya ya Ruto yanakuja siku mbili tu baada ya rais Ruto kunukuliwa akisema kwamab katika serikali yake, yeye atakuwa mstari wa mbele kuonesha njia kwa Wakenya wote kulipa ushuru ili taifa lijitegemee na miaka ijayo tupunguze deni la kitaifa.

Ruto ambaye kando na kuwa mwanasiasa pia ni mjasiriamali katika soko la hisa na pia ufugaji wa kuku aliahidi kuonesha mfano mzuri katika kulipa ushuru ili Wakenya wote kufuata mkondo huo.