Ruto awapongeza wanafunzi wa Kenya kwa kushinda Sh120m Marekani

Muhtasari
  • Ruto awapongeza wanafunzi wa Kenya kwa kushinda Sh120m Marekani
  • Hao ni pamoja na Lennox Omondi, Keylie Muthoni, Dulla Shiltone na Brian Ndung'u
  • Waliibuka kinara wakizishinda timu nyingine tano
Lennox Omondi, Keylie Muthoni, Dulla Shiltone na Brian Ndung'u.
Image: RAIS WILLIAM RUTO/TWITTER

Rais William Ruto amepongeza kundi la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Kenya waliopewa jina la Eco-Bana Limited kwa kushinda fainali za kimataifa za Tuzo ya Hult ya 2022 iliyofanyika New York siku ya Jumanne.

Kundi hilo lilizawadiwa dola milioni moja (Sh milioni 120) kwa uvumbuzi huo.

Ruto alisherehekea kikundi hicho akisema uvumbuzi huo ni roho ya shauku ambayo ana nia ya kuunga mkono.

"Hongera kwa Eco-Bana, mradi wa kijamii wa Kenya ulioanzishwa na wanafunzi wanne wa chuo kikuu, ambao umeshinda Tuzo ya kifahari ya Hult na tuzo ya pesa taslimu ya dola milioni 1," Ruto alisema.

"Tuzo inatolewa kwa wajasiriamali ambao wanajitahidi kukabiliana na masuala ya kimataifa kwa njia ya uvumbuzi. Kampuni inatengeneza pedi za usafi kutoka kwa nyuzi za ndizi. Hii ni Hustler Spirit ambayo tunapenda kuunga mkono."

Wanafunzi wanne kutoka Chuo Kikuu cha St Paul walishindana katika fainali za kimataifa kama Eco Bana Limited.

Hao ni pamoja na Lennox Omondi, Keylie Muthoni, Dulla Shiltone na Brian Ndung'u.

Waliibuka kinara wakizishinda timu nyingine tano.

Kampuni yao inatengeneza pedi za usafi zinazoweza kuoza kwa kutumia nyuzi za ndizi.

Pia husaidia kusimamisha utengenezaji wa plastiki ili kulinda mazingira.