Ekuru Aukot apoteza dadake katika uvamizi wa wezi wa mifugo Turkana

Kiongozi huyo wa Thirdway Alliance aliililia serikali mpya kuhakikisha usalama katika jamii za Kaskazini mwa Kenya dhidi ya wezi wa mifugo.

Muhtasari

• "Tutawazika, lakini turekebishe suala la ukosefu wa usalama Turkana Mashariki,” alitweet Aukot.

Aukot apoteza dadake katika shambulio la wezi wa mifugo
Aukot apoteza dadake katika shambulio la wezi wa mifugo
Image: MAKTABA

Usiku wa Jumamosi taifa lilishtushwa na taarifa za tanzia kutoka Kaskazini mwa Kenya ambapo iliripotiwa watu kadhaa waliangamia katika katika mashambulizi ya watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo

Taarifa hizo zilisema kwamba maafisa watano wa polisi, chifu mmoja na rais mmoja ni miongoni mwa walioangamia katika shambulio hilo amablo limetajwa kuwa baya zaidi katika siku za hivi karibuni.

Sasa imebainika kwamba raia huyo mmoja kwa jina Mary Kanyaman ni dadake kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Aukot alitangaza kwamba dadake ni miongoni mwa 11 walioangamia katika shambulio hilo lililotokea Turkana East siku ya Jumamosi.

Kupitia kwa chapisho la mtandao wa kijamii Jumamosi jioni, Dkt Aukot alisema shambulizi hilo la majambazi lilikatisha maisha ya dadake ambaye sasa amewaacha watoto wadogo kama mayatima.

Aukot aliwalilia rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua na kuwataka kutilia maanani usalama wa watu wa jamii ya Turkna,a Pokot, Samburu miongoni mwa zingine ambazo visa vya mashambulizi ya wezi wa mifugo si jambo geni.

“Mpendwa Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua, nimempoteza dada yangu Mary Kanyaman, mama wa watoto wadogo, aliyeuawa na majambazi wa Pokot huko Napeitom. Pia tumempoteza chifu wa eneo hilo na maafisa wengine 5 wa polisi. Tutawazika, lakini turekebishe suala la ukosefu wa usalama Turkana Mashariki,” alitweet Aukot.

Aidha, tume ya huduma kwa polisi kupitia msemaji wao Bruno Shioso walitoa ripoti kuhusu mauaji hayo na kusema polisi walioangamia walikuwa wakiwafuata wezi wa mifugo walioaminika kutoka jamii jirani ya Pokot.

"Maafisa hao walikuwa katika msako mkali wa kuwasaka majambazi wa Pokot ambao walikuwa wamevamia kijiji kimoja huko Turkana Mashariki na kutorosha mifugo. Chifu wa eneo hilo, watu wawili (2) wa umma na maafisa wanane (8) wa polisi walifariki dunia kutokana na majeraha hayo,” Shioso alisema katika taarifa yake.