Spika Wetang'ula aomboleza kifo cha kaka mkubwa wa DP Gachagua

Awali Gachagua alimuoboleza kakake na kusema kwamba walifurahia pamoja kipindi cha kuapishwa kwake kama naibu rais.

Muhtasari

• Pole sana ndugu yangu,@rigathi ,familia yako yote na marafiki kufuatia kufiwa na wewe kaka mkubwa - Spika Wetang'ula aliandika.

Naibu wa rais Rigathi Gachagua akiwa kati kati ya mkewe na marehemu ndugu yake
Naibu wa rais Rigathi Gachagua akiwa kati kati ya mkewe na marehemu ndugu yake
Image: Facebook

Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula ametuma risala zake za rambi rambi kwa familia ya naibu rais Rigathi Gachagua kwa kumpoteza kaka yake mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Gachagua alitangaza kifo cha nduguye mkubwa na kusema kwamba walishirikiana na kujivinjari maisha mazuri pamoja kipindi cha uhai wake.

"Ndugu yangu mkubwa, Jack Reriani,tulitumia muda bora kwa siku tatu wakati wa uzinduzi wetu.Ulikuwa na furaha sana, mcheshi na umejaa maisha. Sikujua kwamba nyakati hizo nzuri tulizoshiriki zingekuwa za mwisho. Habari za kufariki kwako jana usiku zilinigusa sana huku nikisalia peke yangu miongoni mwa wana Kirigo.Rambirambi zangu za dhati kwa familia yako, familia ya Kirigo, familia kubwa ya Gachagua na familia pana ya Reriani," naibu rais aliomboleza.

Muda mchache baadae viongozi mbali mbali wamejumuika naye kuomboleza kifo hicho cha nduguye ambacho alikitaja kuwa cha ghafla.

"Kumpoteza kaka mkubwa hasa yule aliyechukua nafasi kama ya mzazi ni mojawapo ya mambo yenye kuhuzunisha sana. Pole sana ndugu yangu,@rigathi ,familia yako yote na marafiki kufuatia kufiwa na wewe kaka mkubwa, Mr.Jack Reriani.Bwana akufariji," spika huyo wa nane wa bunge la kitaifa aliomboleza kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kifo cha nduguye kinatokea miezi michache tu baada ya kifo cha ndugu yake mwingine kilichotokea kipindi cha kampeni. 

Jumamosi, Gachagua alikuwa miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria mazishi ya aliyekuwa naibu gavana wa Baringo Charles Kipngok aliyefariki katika uwanja wa ndege wa JKIA wiki moja iliyopita wakijiandaa kuabiri kuenda Mombasa kongamano la magavana.