Kazi ndio hii!: Ruto atoa amri ya kuajiriwa kwa maafisa wa kulinda misitu 3300

Rais alisema mipango hii itafanikisha taifa kufikisha miti bilioni 10 katika miaka 10 ijayo.

Muhtasari

• Tunapanga kukuza miti bilioni 5 katika miaka mitano ijayo na miti bilioni 10 ya ziada kufikia 2032." Ruto alisema.

Rais Ruto atangaza kuajiriwa kwa maafisa wa kulinda misitu
Rais Ruto atangaza kuajiriwa kwa maafisa wa kulinda misitu
Image: Facebook

Rais Ruto ametangaza mpango wake wa kukuza mazingira na kuvutia mvua kwa wingi. Katika hotuba yake siku ya mashujaa katika uwanja mdogo wa Uhuru Gardens, Ruto alisema kwamba azimio lake ifikapo mwaka 2032 ni kuona miti imepandwa zaidi ya bilioni 10 nchini.

Kiongozi huyo wa taifa alisisitiza kujitoea kwake kulinda mazingira ambapo alisema kwamba kila Mkenya mwenye nia njema na mazingira yetu ni anafaa kupanda miti 300 ili kufikisha idadi ya miti bilioni 15 kote nchini, na hivyo kuvutia mvua ambayo maji yake yatatumika kukuza vyakula na kutokomeza kabisa kiangazi.

"Ikiwa tutapanda miti bilioni 15, kila Mkenya atalazimika kukuza miti 300. Tunapanga kukuza miti bilioni 5 katika miaka mitano ijayo na miti bilioni 10 ya ziada kufikia 2032." Ruto alisema.

Rais alitangaza mpango wa serikali yake kuwaandika Wakenya kadhaa kazi katika idara ya misitu ili kuhakikisha huduma kwa misitu inadumishwa na kukomesha visa vya ukataji kiholela wa miti.

Alitoa amri ya kuajiriwa kazi kwa maafisa walinzi wa misitu zaidi ya elfu mbili na mia saba, 2700 pamoja pia na maafisa wa kuhudumu misituni zaidi ya 600.

Hii si mara ya kwanza rais anatoa wito kwa Wakenya kulinda misitu kwani wiki chache zilizopita rais alitoa wito kwa Wakenya kila mmoja kupanda miti 100 katika mashamba yao kama njia moja ya kuafikiana na ruwaza ya mwaka 2030.

"Kila Mkenya, milioni 50 kati yetu, lazima apande miti isiyopungua 100, ama katika boma lako, shambani mwako au katika sehemu nyingine yoyote utakayopata," alisema.