Sina uhakika iwapo bei ya unga itashuka hivi karibuni - Linturi, waziri mteule wa kilimo

Unga nchini kwa sasa unauzwa kwa zaidi ya shilingi 200

Muhtasari

• “Bei ya unga sidhani kama itashuka mara moja isipokuwa serikali ikiwa tayari na iko tayari kuendelea na mpango wa ruzuku - Linturi.

Waziri mteule wa kilimo na Mifugo Mithiki Linturi alisema hana uhakika iwapo bei ya unga itashuka kama inavyotazamiwa na wakenya wengi.

Linturi alisema haya wakati alikuwa akihojiwa na kamati ya Bunge la kitaifa  Ijumaa, kuhusu uteuzi alioupata kutoka kwa serikali ya Rais Ruto.

Linturi alisema bei ya unga itashuka ikiwa serikali itandelea na ruzuku hiyo.

"Bei ya unga sidhani kama itashuka mara moja isipokuwa serikali ikiwa tayari na iko tayari kuendelea na mpango wa ruzuku. Hili ni jambo ambalo litajadiliwa,”  Linturi alisema.

Mnamo Julai mwaka huu rais Rais mstaafu aliwasilisha ruzuku ambayo ilisababisha bei ya unga kushuka hadi shilingi 100. Mpango huu wa ruzuku uliazimia kusaidia kupunguza ghalama ya maisha ambayo imekuwa ikiwaumiza wakenya sana.

Hapo mwanzo Rais mstaafu Uhuru Kenyata alisema mpango wa ruzuku ni wa kusaidia Wakenya wanaoishi kwa mapato ya chini zaidi.

Uhuru akizungumza katika uzinduzi wa ruzuku hiyo mnamo Julai 20 alisema,

"Mpango huu wa ruzuku ya takriban Shilingi 105 kwa mfuko wa kilo 2 ya unga wa mahindi unakusudiwa kupunguza gharama kwa watu wanaishi maisha ya kipato cha chini,  tunapotafuta suluhu la kudumu la kupanda kwa bei ya unga kila uchaguzi,"

Kwenye maduka makuu na ya reja reja bei ya unga imekuwa ikiuzwa kwa shilingi 200 baada ya rais William Ruto kufutilia ruzuku hiyo ya chakula. 

Ruto alisema ruzuku hiyo haikuwa bora na imeshindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa ya kuhakikisha hakuna Mkenya atahujumiwa na hali ngumu ya maisha.

'"Hatutakuwa tukifadhili matumizi, tutafanya kazi na kusaidia wazalishaji," Ruto alisema.