Serikali itahakikisha Usalama wa Wanahabari-Waziri Owalo

Tunaamini ikiwa vyombo vya habari vinawajibika basi vinapaswa kujidhibiti kulingana na sheria za nchi

Muhtasari
  • Wakati huo huo, Owalo alisema atashirikiana na wizara husika kutegua kitendawili cha mauaji ya mwanahabari tajika wa Pakistan
WA

Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali Eliud Owalo ametoa hakikisho kuhusu kujitolea kwa serikali katika kuhakikisha usalama wa wanahabari na kudumishwa kwa uhuru wa vyombo vya habari humu nchini.

Akiongea Jumatano asubuhi katika hoteli moja jijini Nairobi wakati alipokutana na waakilishi wa chama cha wahariri humu nchini pamoja na kundi la kikazi la vyombo vya habari humu nchini wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukomesha ukandamizaji wa wanahabari, Owalo alisema uhalifu dhidi ya wanahabari unatekelezwa na baadhi ya maafisa wa serikali lakini serikali iliyopo itawalinda na kuwasaidia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Wadau wa Vyombo vya Habari wakiongozwa na Chama cha Wahariri wa Kenya walitoa wasiwasi wa usalama kuhusu wanahabari ikiwa ni pamoja na Unyanyasaji wa Kijinsia ulioshuhudiwa wakati wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022.

"Hatuamini katika udhibiti wa vyombo vya habari au kufungwa kwa vyombo vya habari. Tunaamini ikiwa vyombo vya habari vinawajibika basi vinapaswa kujidhibiti kulingana na sheria za nchi na bila shaka maadili yanaelekeza taaluma yako mwenyewe,” Owalo alisema.

Aliongeza: "Wizara yangu na serikali nzima ya Kenya Kwanza itaendelea kutetea uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru mwingine wa kiraia."

Hata hivyo, alitoa wito kwa vyombo vya habari kujidhibiti ifaavyo akisema bodi ya baraza la vyombo vya habari humu nchini itabuniwa haraka iwezekanavyo.

Wakati huo huo, Owalo alisema atashirikiana na wizara husika kutegua kitendawili cha mauaji ya mwanahabari tajika wa Pakistan Arshad Shariff ili kuhakikisha haki itatekelezwa