Gavana Sakaja atoa mpango wa kuwalipa wale watakaoripoti uchafuzi wa mazingira

Sakaja alisema kuwa iwapo utamuona mtu anamwaga taka ovyo na umripoti basi utalipwa kutokana na faini atakayetozwa mchafuzi

Muhtasari

• Sakaja amekuwa na shauku ya kuhakikisha Nairobi inarejea katika hali yake ya usafi baada ya kuwa hali chafu kwa muda mrefu.

Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ametangaza kuwa kaunti ya Nairobi itawalipa watu wanaowakamata wachafuzi wa mazingira kwa kutupa takataka ovyo katika mitaa ya mjini.

Akitoa tangazo hilo kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii, Sakaja alisema kuwa serikali yake kwanzia sasa itachukua jukumu la kuwalipa watu wanaowatumbua wale wanaotuoa taka ovyo.

Sakaja aliwataka wana Nairobi wote kuwa macho na pindi watakapowaona watu wakirundika takataka kwa umma wawaripoti kwa mamlaka za kaunti na pindi watakapofikishwa mahakamani basi faini watakayotozwa itagawanywa pasu kwa pasu baina ya kaunti na mfichuzi.

"Tunapofungua mfumo wa mifereji ya maji katika jiji lote, hebu tuache utupaji taka haramu zaidi. Ukiona mtu akirundika takataka ovyo, mrekodi, mlika kabisa; tunakamata, tunashtaki na tunagawanya faini. Itafanya kazi kwa sheria ya kaunti ili kutoa hii. Tufanye jiji letu kuwa safi," gavana Sakaja alisema.

Sakaja amekuwa na shauku ya kuhakikisha Nairobi inarejea katika hali yake ya usafi baada ya kuwa hali chafu kwa muda mrefu.

Jijini Nairobi, watu wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu si tu kufuatia uchafuzi wa mazingira kwa mirundiko ya taka bali pia ukosefu wa njia mbadala za wapiti njia kwa miguu na vile vile mifereji ya kupitisha maji taka ni tatizo sugu.

Zaidi ya hayo, mapipa ya takataka ambayo yaliwekwa kimkakati sasa hayapo, na yale machache yanayopatikana yako mbali sana. Hata kwa machache yanaopatikana, mengine yako katika hali duni.

Siku mbili tu baada ya kuapishwa kama gavana wa Nairobi, Sakaja, pamoja na naibu wake James Muchiri walizuru sehemu mbalimbali za jiji.

“Nimetoa maagizo madhubuti ambayo yatahakikisha kusuluhisha tatizo la sasa la takataka kote jijini. siku chache zijazo.Tunataka kuona jiji la utaratibu, utu, matumaini na fursa kwa wote” Sakaja alisema.