Sakaja kukutana na IG Koome,kushiriki suluhu za kuleta usalama Nairobi

Majambazi jijini Nairobi wameripotiwa kufikia hatua kali za kuwadunga visu waathiriwa wao ili kuwaibia.

Muhtasari
  • Haya yanajiri huku kukiwa na ongezeko la visa vya uhalifu jijini Nairobi
  • Kesi za  wizi kwa kutumia vurugu zimeongezeka
  • Majambazi jijini Nairobi wameripotiwa kufikia hatua kali za kuwadunga visu waathiriwa wao ili kuwaibia
GAVANA WA NAIROBI JOHNSON SAKAJA
Image: SAKAJA/TWITTER

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja atakutana na Inspekta Jenerali mpya wa Polisi, Japheth Koome ili kuzungumza kuhusu masuala ya usalama katika jiji kuu.

Sakaja alisema wawili hao watashiriki suluhu za kurejesha usalama Nairobi.

Gavana huyo hakufichua siku au tarehe ya mkutano wao.

"Nimezungumza na Inspekta Jenerali wa polisi. Tumekubaliana kukutana na kubadilishana suluhu na kazi katika kurejesha utulivu na usalama,” alisema.

Gavana huyo alisema ingawa usalama ni kazi ya kitaifa, serikali ya kaunti itaingilia kati ili kuunga mkono wasimamizi wa sheria.

"Ni jukumu letu la pamoja. Tutaunga mkono maafisa wetu wanapolinda watu wetu,” Sakaja alisema.

Haya yanajiri huku kukiwa na ongezeko la visa vya uhalifu jijini Nairobi.

Kesi za  wizi kwa kutumia vurugu zimeongezeka.

Majambazi jijini Nairobi wameripotiwa kufikia hatua kali za kuwadunga visu waathiriwa wao ili kuwaibia.

Daktari kutoka Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta hivi majuzi alitumia mitandao ya kijamii kuwaonya raia kuhusu ongezeko la wagonjwa wanaolazwa wakiwa na majeraha ya visu kutokana na wizi.

Koome aliapishwa siku ya Ijuuma kuwa inspekta jenerali wa polisi, huku hafla hiyo ikiongoza na jaji mkuu Martha Koome.