Anne Waiguru akutana na Bill Gates amsawishi kufadhili miradi muhimu

Hata hivyo, alitoa wito wa kuungwa mkono katika mipango hiyo ili kuhakikisha kuwa mpango huo unanufaisha

Muhtasari
  • Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya Bill Gates nchini Kenya. Aliwasili nchini Jumanne, Novemba 15 kwa ziara ya wiki moja
GAVANA ANNE WAIGURU NA BILIONEA BILL GATES
Image: ANNE WAIGURU/TWITTER

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru mnamo Alhamisi, Novemba 17, aliupongeza Wakfu wa Bill Gates kwa msaada katika uboreshaji wa huduma za afya kwa Wakenya.

Waiguru, ambaye alizungumza wakati wa mkutano kati ya Baraza la Magavana na Wakfu wa Bill Gates alibainisha kuwa machifu wa kaunti walijitolea kutekeleza mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote.

Hata hivyo, alitoa wito wa kuungwa mkono katika mipango hiyo ili kuhakikisha kuwa mpango huo unanufaisha watu katika ngazi ya kaunti.

Huku akiangazia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya tangu kuja kwa ugatuzi, Waiguru alibainisha kuwa kuongezwa zaidi kwa huduma za afya kwa jamii kutasaidia katika kupunguza changamoto za kiafya.

Waiguru pia aliangazia mimba za utotoni kuwa kero kuu kwa magavana na kuomba ushirikiano kutoka kwa Wakfu wa Bill Gates ili kuhakikisha kuwa vijana walioathiriwa wanapata nafasi ya kurejea masomo yao.

"Aliomba kuungwa mkono katika programu za utetezi wa Afya ya Uzazi ili kupunguza mimba za mapema  pamoja na msaada katika uanzishwaji wa nyumba za kulelea watoto ambapo kina mama vijana wanaweza kuwaacha watoto wao wakitafuta elimu."

Maeneo mengine ya uwezekano wa ushirikiano yaliyosisitizwa na Gavana ni pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii, wakunga wa jadi na kupitia teknolojia kama vile uchunguzi wa ultrasound na matumizi ya akili bandia.

Mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya Bill Gates nchini Kenya. Aliwasili nchini Jumanne, Novemba 15 kwa ziara ya wiki moja.

Mkubwa huyo wa biashara wa Marekani alikutana na Rais William Ruto na wakakubaliana kushirikiana katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Bill Gates pia alizuru Kaunti ya Makueni ambapo alifanya mkutano na gavana wa eneo hilo.