Bungoma: Mwanaume achomwa kwa maji moto na mwanamke kwa kumuibia

Mwanamke alimchoma na maji aliyokuwa amechemsha kwenda kuoga bafuni

Muhtasari

• Mwanamke huyo alimumwagilia maji moto yaliokuwa kwenye besheni alipokuwa ameenda bafuni kuoga.

• Alipigwa kitutu na wanakijiji waliokuwa wamepandwa na mori.

• Mshukiwa huyo anapigania maisha yake katika hospitali ya rufaa huko Bungoma.

Maji moto
Maji moto
Image: BBC

Mwamamume mmoja anauguza majeraha katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Bungoma baada ya kuchomwa na maji moto akijaribu kuiba nyumbani katika kijiji cha Tuuti.

Kulingana na maafisa wa kupambana na makosa ya jinai DCI, mshukiwa huyo wa ujambazi ambaye hakutambulishwa kwa jina alikuwa ameingia nyumbani mwa Zipporah Masika alipokuwa akijiandaa kwenda kuoga.

Masika, Alhamisi, majira ya saa tano asubuhi alikuwa amechemsha maji ya kwenda bafuni kuoga kabla ya kupatana na mwizi wakikodoleana naye macho akiwa amebeba simu yake mkononi na vitu vingine vya thamana baada ya kupora nyumba.

Jambazi huyo aliingia taabani na kujipata pabaya  baada ya Masika kumwangilia maji moto yaliokuwa kwenye besheni baada ya kujaribu kutoroka bila mafanikio. Kwa uchungu mwanamume huyo alilia na kuwika kwa lugha ya mama baada ya uso wake kuharibiwa na maji moto.

Mshukiwa wa wizi aliuguza majeraha mabaya huku akiwavutia majirani kutokana na kamsa aliyokuwa ameipiga kwa maumivu.

Baada ya kupata upenyo wa kutoka nje majirani waliokuwa wamefika na kupandwa na mori huku wakianza kuchukua sheria mikononi mwao kumwadhibu kwa makofi na mateke.

Mshukiwa huyo alijaribu kuomba raia wamsamehe ila ombi lake halikukubaliwa wala hakusamehewa huku akipigwa kitutu.

Ripoti ya DCI kwenye ukurasa wao wa Facebook ilisema '' Wakati maafisa wa polisi walipofika, mwanamume huyo alikuwa amevujwa na damu kutokana na kupigwa na wanakijiji wenye hasira ambao walikuwa wamefika kwa wingi.''

Jamaa huyo anaendela kupokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Bungoma ambapo kwa sasa anapigania maisha yake.

Licha ya hayo DCI iliwaomba wananchi kuwa watulivu kitendo kama hiki kinapojiri na wanashauriwa kutojichukulia sheria mkononi mwao, bali watoe ripoti kwa maafisa wa polisi ili sheria ichukue mkondo wake dhabiti.