Jinsi juhudi za mwanamke za kupenyeza bangi kwa mumewe gerezani zilivyositishwa

Mwanadada huyo alikuwa ameficha bangi na sigara kwenye mkate na ndani ya suruali yake.

Muhtasari

• Mwanadada anazuwiliwa kwenye kituo cha polisi cha Gilgil huku uchunguzi zaidi dhidi yake ukiendelea.

• Mwanadada huyo alijaribu kuwahonga maafisa wa polisi kwa shilingi 2,000.

Image: Facebook//DCI

Mwanamke mmoja anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Gilgil baada ya kupatikana akijaribu kupeleka bangi kwa mumewe aliyekuwa amekamatwa.

Caroline Imenza mwenye umri wa miaka 30 alifika kituoni mnamo Jumapili, Novemba 27 majira ya asubuhi na kuomba kumwona mumewe Stephen Nyabuto ambaye alikuwa anazuiliwa.

Imenza, ambaye kwa mtazamo tu hangeshukiwa kuwa na mipango mingine ya kando alikuwa amebeba mkate na kibuyu kilichojaa chai moto, ili mumewe akabadhiwe kama kiamsha kinywa chake.

Kulingana na ripoti ya DCI, afisa wa polisi aliyekuwa katika zamu wakati huo aliamua kuufungua mkate huo na kupata misokoto mitano ya bangi, sigara tano na kiberiti katikati ya mkate huo.

Bila kusita, afisa huyo alimkamata mwanadada huyo na kumfungia kwenye seli kabla ya  uchunguzi wa kina kufanyika. Mshukiwa pia alipatikana na bangi misokoto 80 mingine ya bangi  kwenye suruali yake ya ndani.

Juhudi za mshukiwa za kuwahonga maafisa hao kwa shilingi 2,000 ili kuachiliwa ziliangulia patupu. 

''Tunapopongeza hatua ya afisa wa polisi aliyekuwa kwenye zamu na wenzake, mtuhumiwa kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha Polisi huku akisubiri kufikishwa mahakamani''ripoti ya polisi ilisema.