Vihiga: Wakulima kuuziwa mbolea ya kinyesi cha binadamu kwa ksh 300 kwa mfuko

Gavana Wilberforce Ottichilo alisema mpango huo utaimarisha kilimo.

Muhtasari

• Mradi huu uliogharimu shilingi milioni 17 unapania kutengeneza mbolea ya bei nafuu na kuimarisha kilimo.

Image: BBC

Serikali ya kaunti ya Vihiga ilizindua mradi ambao utasaidia katika kutengeneza mbolea ya bei nafuu inayotokana na kinyesi cha binadamu ili kuwaepusha wakulima dhidi ya bei ya juu ya mbolea bandia na kuimarisha kilimo eneo hilo.

Kituo hicho cha kuhifadhi kinyezi hicho kilichoko mji wa Mbale na kilichogharimu shilingi milioni 17 kitakuwa kinakusanya kinyesi cha binadamu huku kikitoa magari sita ya exhauster yakubebea kinyesi hicho.

Mkurugenzi wa usafi wa mazingira katika kaunti ya Vihiga James Odiero alisema mbolea kutoka kwa kinyesi cha binadamu itauzwa kwa wakulima kati ya shilingi  300 hadi shilingi 500 kwa mfuko.

Mladi huu ambao ulianza mwaka wa 2020 na kuchukua miaka miwili kukamilika Bwana Odiero alisema  "Kupitia mradi huu, tutasafisha kinyesi kutoka kwa vyoo na kisha kukitengeneza kuwa mbolea ambayo itauzwa kwa wakulima."

"Hili litarudishia faida zilizotumika kujenga mradi huo. Kila siku tutasafisha cubu 50 za kinyesi hicho ambayo ni sawa na lita 50,000 za takataka zilizotolewa na mashine sita za exhauster," alifafanua.

Gavana Wilber Ottichilo alisema mpango  huo utaimarisha kilimo na pia utasaidia katika kuzima utamaduni  wa wanajamii wanao jenga vyoo kila mara.

"Mradi huu utasaidia kusafisha mazingira yetu na kuziba uharibifu wa kila namna wa mazingira."  Ottichilo alisema.