Mmepiga 'wrong number' - waziri Kindiki awaonya wahalifu

Tutawatafuta katika maficho yenu, hatutasubiri hata mvamie watu - Kindiki.

Muhtasari

• Waziri alikuwa akiwauliza watu katika jiji la Nairobi kuhusu hali ya usalama kwa wiki mbili tangu maafisa waanze kupiga patroli.

Waziri Kindiki akikagua baadhi ya silaha za polisi
Waziri Kindiki akikagua baadhi ya silaha za polisi
Image: Facebook

Baada ya wiki kadhaa za kujaribu kudhibiti jiji la Nairobi kutokana na visa vya wizi wa kimabavu kutoka kwa magenge hatari ya vijana, waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki amefanya ziara ya ghafla kwenye baadhi ya maeneo katikati mwa jiji la Nairobi ili kujua kama hatua za kiusalama zimezaa matunda.

Waziri Kindiki alisema kuwa hali imekabiliwa vilivyo na maafisa wa polisi wengi ambao wamekuwa wakipiga patrol katika maeneo mbali mbali wakiwa katika mavazi ya kiraia.

Akizungumza siku ya Jumatatu baada ya kutathmini hali ya usalama katika eneo la CBD, Prof Kindiki alisema visa vya ukosefu wa usalama vimepungua katika wiki iliyopita.

"Ripoti tuliyonayo hadi sasa ni kwamba kwa wiki iliyopita, hali ya kawaida imerejea. Hatujasikia uhalifu ulioripotiwa, hasa wizi na watu kushambuliwa kwa silaha za moto na visu,” alisema.

Waziri huyo alisema alipokuwa akishirikiana na wafanyabiashara na Wakenya katika CBD, alipata ripoti nzuri kutoka kwao.

"Ninataka kuthibitisha kwa uthabiti na bila shaka kwamba serikali inafanya chochote kinachohitajika ili kuhakikisha kuwa raia wanalindwa dhidi ya wahalifu."

Kindiki alisisitza msimamo wa serikali kuwa haiku tayari hivi karibuni kuwaachia wahalifu hao kuliteka jiji hata kidogo kwani serikali imesimama tisti na imara kukabiliana nao hadi pale watakapokubali kuwa wizi haulipi kabisa.

“Ikiwa mnafikiri mna silaha za kutosha na mbinu za kutosha kukabiliana na serikali, nataka niwahakikishie kuwa mmepiga namba isiyo sahihi. Tutawatafuta katika maficho yenu, hatutasubiri hata mvamie watu, tutaondoa mashambulizi,” Prof Kindiki alisema.