Kampuni ya teksi za umeme ya NopeaRide imesitisha huduma zake Kenya

Kuondoka kwao Kenya kunafuatia wenye hisa wakuu kutoka Finland kutangazwa kufilisika.

Muhtasari

• Tungependa kutoa masikitiko yetu makubwa kwa timu yetu iliyojitolea ya wafanyikazi na madereva - taarifa ilisema.

Kampuni ya teksi za umeme ya Nopea
Kampuni ya teksi za umeme ya Nopea
Image: FaCEbook

Kampuni ya teksi za kutumia umeme ya NopeaRide imetangaza kuondoka katika soko la kutoa huduma zao kwa Wakenya.

Kufuatia taarifa ambayo walichapisha kwenye tovuti yao, NopeaRide ilisema hatua hiyo ya kuondoka katika soko la kutoa huduma za teksi nchini inafuatia wawekezaji wao wakuu wa hisa kutoka nchini Finland kutangazwa kuwa wamefilisika.

“Kufuatia tangazo kwamba mwenyehisa wetu aliye na hisa nyingi, EkoRent Oy, ametangaza kuwa amefilisika nchini Ufini, tunasikitika kutangaza kwamba InfraCo Africa Limited mwenye hisa ndogo sasa amewasilisha kesi ya kufutwa kwa EkoRent Africa Limited katika Mahakama Kuu ya Kenya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba EkoRent Oy alikuwa mfadhili mkuu wa EkoRent Africa Limited na ujuzi wote wa kiufundi kuhusu uendeshaji wa biashara hiyo ulikuwa na EkoRent Oy,” kampuni hiyo ilitangaza.

Walitangaza kuwa wameondoa magari yao yote barabarani mara moja na tayari taarifa hiyo imesambazwa kwa wahudumu wao wote, huku shughuli za mamlaka husika zikiendelea ili kufanikisha hatua zote.

“Tungependa kutoa masikitiko yetu makubwa kwa timu yetu iliyojitolea ya wafanyikazi na madereva. Tungependa pia kuwashukuru wateja wetu waaminifu wa NopeaRide, wateja wa kampuni na washirika wengine ambao wameunga mkono maono ya NopeaRide ya umeme barani Afrika,” walisikitika.

Kuondoka kwa kampuni hiyo katika soko la Kenya kunafuatia hali ngumu ya kiuchumi inayoendelea kuwatesa Wakenya wengi huku biashara nyingi pia zikiripotiwa kuanguka.

Mapema mwaka huu, kampuni ya hoteli kubwa ya Hilton ilitangaza kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, hoteli yao kubwa iliyoko katikati mwa jiji la Nairobi itafungwa rasmi kutokana na kushindwa kujirudi shughuli zao za kawaida tangu kulemazwa na janga la Korona.