Francis Gachuri atoa taarifa ya kibinafsi baada ya tukio la sumu kwenye chakula RMS

Waruru aliongeza kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikichukua hatua kuhakikisha tukio kama hilo halijitokezi tena.

Muhtasari
  • Gachuri kwenye mtandao wake wa kijamii alisema alikuwa vyema akiongeza kuwa suala hilo lilikuwa likishughulikiwa kwa weledi
FRANCIS GACHURI
Image: FRANCIS GACHURI/FACEBOOK

Mhariri wa Masuala ya Kisiasa ya Citizen TV Francis Gachuri ametoa taarifa ya kibinafsi kufuatia kisa cha sumu iliyokuwa kwa chakula katika afisi za Royal Media Services (RMS).

Kisa hicho ambacho kilisababisha kifo cha mfanyakazi mmoja kilitokea mnamo Desemba 26, 2022, na kuathiri wafanyikazi wanaofanya kazi zamu ya Krismasi.

Gachuri kwenye mtandao wake wa kijamii alisema alikuwa vyema akiongeza kuwa suala hilo lilikuwa likishughulikiwa kwa weledi.

"Asanteni nyote kwa simu zenu, SMS na kujali fadhili. mimi ni mzima. Pole kwa familia ya mwenzetu aliyefariki. Kila la heri na ahueni ya haraka kwa wenzetu wanaopata nafuu. Hali ya sumu ya chakula inashughulikiwa kitaalamu na kwa uangalifu wa hali ya juu. Iko vizuri,” alibainisha.

Akizungumzia kisa hicho, Mkurugenzi Mkuu wa RMS Wachira Waruru alisema kampuni hiyo ilikuwa ikitoa usaidizi unaohitajika kwa wafanyikazi walioathiriwa.

Waruru aliongeza kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikichukua hatua kuhakikisha tukio kama hilo halijitokezi tena.

Akithibitisha kifo cha mmoja wa wafanyakazi hao, Waruru alitoa pole kwa familia ya marehemu, na kutuma ujumbe wake wa kuwatakia heri wapendwa wao.

“Tumeshtushwa na kuhuzunishwa sana kuwafahamisha umma kuwa mfanyakazi mmoja amefariki kwa bahati mbaya kutokana na ugonjwa unaodhaniwa kuwa ni sumu kwenye chakula. Mawazo na sala zetu ziko pamoja na familia ya mfanyakazi wetu aliyefariki katika kipindi hiki kigumu," Wachira alisema.