KMTC yazindua mafunzo ya diploma katika Sayansi ya kuhudumia Maiti

Kozi hiyo itachukua miaka 3 na mafunzo yanaanza rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Muhtasari

• "Ni kozi ya kwanza kabisa katika Afrika Mashariki na Kati,” sehemu ya taarifa yao ilisoma.

Makafani ya Nairobi
Makafani ya Nairobi
Image: makafani,

Chuo anuwai cha mafunzo ya matibabu cha Kenya KMTC kimetangaza kuwa kimeanzisha taaluma ya kufunza watu jinsi ya kushughulikia miili ya watu wafu katika makafani.

Katika taarifa rasmi ambayo walitoa kweney ukurasa wao wa Twitter, chuo hicho kilitangaza kuwa ni ombi ambalo limekuwa likitolewa na waru wengi ambao wamekuwa wakitaka kujishughulisha na kuhudumia wafu lakini wanashindwa pa kuanzia.

Walisema kuwa mafunzo hayo ambayo ni diploma katika sayansi ya mochwari yataanza kufunzwa rasmi mwezi Machi mwaka huu huku wakitamba na kujigamba kuwa ndio watakuwa wa kwanza kutoa mafunzo kama hayo ya kipekee katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.

“Mlituuliza, nasi tukasikiliza! Chuo sasa kitakuwa kikitoa Diploma ya Sayansi ya Maiti kuanzia Machi 2023. Ni kozi ya kwanza kabisa katika Afrika Mashariki na Kati,” sehemu ya taarifa yao ilisoma.

Kulingana na taarifa yao, kozi hiyo itakuwa inachukua muda wa miaka mitatu na mtu akitoka hapo hana woga kuhusu kukaribia maiti wala kutagusana nao, kama ambavyo ni kawaida ya watu wengi kuogopa kukaribia hata milango ya makafani.

Walitoa tovuti ya kuwawezesha wale wanaotaka kujiunga na mafunzo hayo kutuma maombi ya kupewa idhini ya kujiunga nao kuanzia Machi.

“Mafunzo haya yanachukua miaka 3, wakati wale ambao tayari wana cheti katika kozi sawa kutoka kwa taasisi zingine zinazojulikana watajiunga mwaka wa pili. Maombi ya kujiunga kuanzia Machi yako wazi na yanaendelea,”       KMTC walisema kupitia kurasa zao rasmi mitandaoni.