Hatumtambui Ruto kama Rais wa Kenya-Raila Odinga

" Kulingana na data ya mtoa taarifa wa IEBC, tulishinda kwa kura zaidi ya milioni 2. Watu wa mlimani walitupigia kura kama ambavyo hawajawahi kufanya hapo awali

Muhtasari
  • Hivyo Raila amewaambia Wakenya wote kuwa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Alliance haumtambui rais wa Kenya Mheshimiwa William Samoei Ruto kuwa rais wa Kenya
KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: ANDREW KASUKU

Baada ya kurejea nchini kutoka Afrika Kusini na kuelekea katika uwanja wa Kamukunji ambapo ametoa hotuba yake kwa Wakenya,kinara wa muungano wa Azimio One Kenya Raila Odinga amesema kwamba hamtambui Rais Ruto kama Rais wa Kenya.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya amewaeleza Wakenya kuwa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kutangazwa tarehe 15 Agosti 2022 walifanya uchunguzi wao na kubaini kuwa alishinda kwa zaidi ya kura Milioni 8.

Hivyo Raila amewaambia Wakenya wote kuwa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Alliance haumtambui rais wa Kenya Mheshimiwa William Samoei Ruto kuwa rais wa Kenya.

Waziri Mkuu huyo wa zamani pia amefahamisha Wakenya kwamba hawatambui maafisa wowote ambao wako afisini kwa sasa.

" Kulingana na data ya mtoa taarifa wa IEBC, tulishinda kwa kura zaidi ya milioni 2. Watu wa mlimani walitupigia kura kama ambavyo hawajawahi kufanya hapo awali. Nataka kuwashukuru wenyeji wa mlima huo kwa kunipa nafasi isiyoweza kushindwa katika uchaguzi...Sisi kama Azimio tunakataa matokeo ya uchaguzi wa 2022. Hatuwezi na hatutatambua utawala wa Kenya Kwanza na kuchukulia serikali ya Kenya Kwanza kuwa haramu. Hatumtambui Bw. William Ruto kama Rais wa Kenya,"Alisema Raila.