Matiang'i aliharibu sekta ya elimu-Aliyekuwa mkuu wa KNUT Sossion adai

Sossion alisema zaidi kwamba serikali lazima iwe na mjadala wa kina kuhusu madhumuni ya mitihani ya kitaifa.

Muhtasari
  • Pia alidai sera za Matiang'i ni za kubana kimakusudi uhamisho wa wanafunzi hadi chuo kikuu
Wilson Sossion
Image: KWA HISANI

Akizungumza wakati wa mahojiano na runinga ya Citizen siku ya Jumatatu, aliyekuwa mkuu wa KNUT Wilson Sossion alisema Matiang'i aliendeleza utamaduni wa kuharibu sekta ya elimu kupitia sera zake.

“Matiang’i alitukuzwa huku akiendeleza utamaduni wa kuwaharibu wanafunzi wetu kupitia sera zake,” alisema Sossion.

Pia alidai sera za Matiang'i ni za kubana kimakusudi uhamisho wa wanafunzi hadi chuo kikuu.

“Tunaharibu wanafunzi wetu kwa mfumo wa gredi,” alisema.

Sossion alisema zaidi kwamba serikali lazima iwe na mjadala wa kina kuhusu madhumuni ya mitihani ya kitaifa.

"Lazima tujadili na kujadili madhumuni ya mitihani ya Kitaifa, tunapaswa kujua kuwa mitihani ipo ili kuwezesha mabadiliko," aliongeza.

Sossion alisema mabadiliko ya wanafunzi katika chuo kikuu bado ni ya chini, akiongeza kuwa inapaswa kuwa sawa na kile kinachotokea kwa wanafunzi wa shule za msingi wanapohamia shule za upili.