Tuju azungumzia nyakati zake za mwisho na Magoha

Tuju alisema waziri huyo wa zamani wa elimu alionekana sawa alipomtembelea nyumbani kwake Lavington

Muhtasari
  • Tuju aliongeza kuwa Magoha alimwambia tu kwamba alikuwa amechoka kidogo baada ya siku ndefu ya kupanga mazishi ya Nyabera
RAPHAEL TUJU NA NDUGUYE GEORGE MAGOHA,JOSEPH MAGOHA
Image: ANDREW KASUKU

Raphael Tuju amesema hakukuwa na dalili zozote kuwa marehemu George Magoha alikuwa mgonjwa alipokuwa naye siku ya Jumatatu.

Tuju alisema waziri huyo wa zamani wa elimu alionekana sawa alipomtembelea nyumbani kwake Lavington, Nairobi kwa ajili ya maandalizi ya mazishi ya marehemu kakake, Richard Alex Nyabera.

"Sikujua kwamba wakati ujao ningezuru nyumbani ingekuwa kwa sababu ya kifo chake," alisema.

Tuju alisema hayo nyumbani kwa Magoha ambako alikuwa ameenda kufariji familia kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Elimu Jumanne.

Wageni katika nyumba hiyo walipokelewa na mjane, Barbara Odudu na mtoto wa kiume Michael Magoha.

Tuju aliongeza kuwa Magoha alimwambia tu kwamba alikuwa amechoka kidogo baada ya siku ndefu ya kupanga mazishi ya Nyabera.

“Mimi kama mwenzangu nimesikitishwa sana na msiba huo, naiombea familia kwa sababu ni wakati mgumu sana kwao,” aliongeza.

Magoha aliaga siku ya Jumanne baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.