ODM yawasuta viongozi wa Luo, Nyanza baada ya kukutana na Ruto Ikulu

Etale alitaja mikutano ya Ikulu kama mbinu ya kugeuza mawazo ya taifa kutoka kwa gharama ya juu ya maisha

Muhtasari
  • "Chama kimekuwa kikifuatilia kwa karibu shughuli zinazohusisha baadhi yao na leo ilikuwa kilele tu," alisema katika taarifa yake

ODM imekashifu wabunge wake tisa kwa kufanya mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu Jumanne asubuhi.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa chama Philip Etale alisema kuwa mkutano wa wabunge haukuwashangaza wao na Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.

"Chama kimekuwa kikifuatilia kwa karibu shughuli zinazohusisha baadhi yao na leo ilikuwa kilele tu," alisema katika taarifa yake.

Mapema Jumanne, wabunge tisa kutoka Nyanza walifanya mkutano na Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Wabunge hao ni pamoja na;Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Shakeel Shabir (Kisumu Mashariki, Independent) Felix Odiwuor almaarufu Jalang'o (Lang'ata), Paul Abuor ( Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Etale alitaja mikutano ya Ikulu kama mbinu ya kugeuza mawazo ya taifa kutoka kwa gharama ya juu ya maisha, ada za shule zisizostahimilika kwa watoto wao na ufisadi.

"Miezi mitatu iliyopita, uongozi wa Azimio la Umoja ulianza mikutano ya kushinikiza kurejeshwa kwa ushindi wake kutoka kwa utawala haramu ili kutoa uongozi ambao Wakenya wanataka, lakini wakati wote, tulijua adui hatakaa vizuri," Etale alisema.